Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Tawi lake la Bonyokwa mkoani Dar es Salaam, kimemvua rasmi uanachama, John Mrema, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu, dharau kwa mamlaka halali za chama, na kukaidi misingi na maadili ya chama.
Kwa mujibu wa barua rasmi iliyoandikwa na kusainiwa Aprili 30, 2025 na Katibu wa Tawi, Solomini Kagaruki, ambayo Jambo TV tumepata kuiona, na ambayo ilitolewa na tawi hilo, Kamati Tendaji ya tawi hilo ilikutana Aprili 29, 2025 na kupitia tuhuma dhidi ya Mrema, kisha kufikia uamuzi wa pamoja wa kumvua uanachama wake kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA @ChademaTz ya mwaka 2006, toleo la 2019, ibara ya 5.4.3.
Miongoni mwa tuhuma zilizomkabili Mrema @JonMrema , aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, ni pamoja na dharau dhidi ya mamlaka za chama ambapo imeelezwa kuwa alisambaza barua ya wito ya kufika mbele ya kamati ya nidhamu kwenye mitandao ya kijamii badala ya kuitikia kwa utaratibu wa chama, jambo lililotafsiriwa kuwa ni dharau kwa mamlaka husika.
Tuhuma nyingine ni kukaidi maadili na misingi ya chama, ikielezwa kuwa akiwa bado katika mchakato wa kujieleza, alifanya mkutano na waandishi wa habari Aprili 22, 2025 na kutoa tuhuma hadharani dhidi ya chama chake, akibeza misimamo na programu za CHADEMA kinyume cha utaratibu wa ndani wa chama.
Barua hiyo imeeleza kuwa, kutokana na mienendo hiyo, Mrema amepoteza sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CHADEMA kuanzia tarehe 30 Aprili, 2025. Hata hivyo, amepewa haki ya kukata rufaa kwa ngazi ya juu endapo hataridhika na uamuzi huo.