Na mwandishi wetu Dar es salaam
Mkuu wa Wilaya Ubungo Mhe. Lazaro Twange amewahakikishia Wananchi wa Mtaa wa Saranga Mpakani, kuwa ifikapo mwezi Machi 2025 wataanza kupata huduma ya maji na kuondokana na changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu .
DC Twange ametoa ahadi hiyo leo Februari 8, 2025 wakati alipofanya Ziara ya kutembelea mtaa huo wa Saranga eneo la Mbuguli ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na kumuelekeza Meneja wa Dawasa kanda ya Kinyerezi kushugulikia swala hilo kwa haraka .
Pia Mhe. DC amemuagiza Meneja wa Dawasa kanda ya Kinyerezi na Uongozi wa mtaa kuzungukia nyumba ambazo wamejiunganishia maji bila kufuata utaratibu na kusababisha wananchi wengine kukosa huduma ya maji ili marekebisho yafanyike ili wananchi wengine wanaokosa maji waweze kupata huduma hiyo ya maji, kwasasa wananchi wanapata huduma hiyo ya maji kupitia Matanki ambayo yanajazwa maji na Dawasa.
Kwa upande wake Meneja wa Dawasa kanda ya Kinyerezi Crossman Makere alieleza kuwa changamoto ya maji katika mtaa huo anaifahamu na imeanza kufanyiwa kazi, ambapo zoezi la ulazaji wa Mabomba linaendelea ambapo mpaka sasa wameshafanikiwa kulaza Mabomba Kilomita tatu toka chanzo kilipo na zimebakia Kilomita tatu mpaka kufika eneo husika.
Makere amesema kuwa mradi huo wa Maji unaotekelezwa katika Kanda hiyo utakamilika machi 2025 na wananchi wataanza kupata maji kwani Serikali imeshaleta fedha kwaajili ya ukamilishaji wa mradi huo.
Aidha meneja huyo ameendelea kufafanua kuwa katika utekelezaji wa mradi huo kuwa mpaka sasa Tanki lenye uwezo wa kubeba maji Lita Milioni tisa limeshajengwa eneo la Bangulo, ambalo litasaidia kusambaza maji katika mtaa wa Saranga na maeneo jirani na kumaliza changamoto ya mgawo.
Pamoja na changamoto ya maji Wananchi wa Mtaa wa Saranga wamemwomba Mhe. DC kushugulikia changamoto ya Ubovu wa Barabara, Ujenzi wa Kituo cha polisi, na Ujenzi wa zahanati na Mhe DC ameahidi kutatua kero hizo kwa kushirikiana na wataalamu.