Saturday, February 8, 2025

BUGANDIKA SEKONDARI WAJA NA MIKAKATI KUFUTA DARAJA 0




Na Lydia Lugakila - Misenyi.

Kufuatia kasoro iliyotokea katika matokeo ya kidato cha pili kwa mtihani wa Taifa 2024/2025 na kusababisha  shule ya Sekondari Bugandika iliyopo Wilayani Misenyi Mkoani Kagera kutofanya vizuri  kamati ya shule Wazazi na Walimu wameamua kukutana na kufanya kikao cha chenye lengo la kuwekeana mikakati mipya ya kitaaluma inayoenda kufuta Daraja la mwisho kwa wanafunzi hao.

Akisoma taarifa ya shule mkuu wa shule hiyo Aron Simon Shalla mbele ya Wazazi amesema wao  kama walimu hawakufurahishwa na matokea ya mtihani wa kidato cha pili yaliyopita hivyo wameamua kuja ki vingine ili changamoto hiyo kuitokomeza kabisa.

"Wazazi mtakumbuka mtihani wa Taifa Mwaka 2024/2025 Daraja la kwanza tulizalisha wanafunzi 3 daraja la pili wanafunzi 2 daraja la tatu wanafunzi 9 Daraja la nne wanafunzi 77 Daraja la mwisho 50 hivyo hatukupendezwa na hali hiyo tumejipanga sasa na  tunasema hatuhitaji tena daraja la mwisho ndo maana mtihani wa kidato cha nne tumefanya vizuri" amesema  Mwalimu Aron.

Aron akiitaja mikakati hiyo mipya mbele ya Wazazi amesema kuwa ni pamoja na kutoa mazoezi ya kila siku na kufanya masahihisho kwa madarasa ya mitihani hii itafanyika kupitia kambi zilizopo shuleni hapo, kupunguza baadhi ya masomo kwa wanafunzi wenye uwezo mdogo ili wapewe masomo kidogo ambayo wana uwezo na uelewa nayo, uendelezaji wa kambi za kitaaluma, kudhibiti utoro, kupata majaribio na mazoezi ya mitihani mbali mbali kutoka shule tofauti za nje ya Wilaya hadi mkoa zinazofanya vizuri, Wanafunzi wote wa kidato cha nne kusoma masomo ya ziada, kusimamia na kuhakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote.

Mkuu huyo wa shule amewaomba wazazi kushirikiana na walimu hao ili kufanikisha mipango hiyo itakayosaidia kuondoa daraja 0 ambapo ameongeza kuwa licha ya mikakati hiyo mipya bado shule hiyo inakumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo baadhi ya Wazazi kutozingatia suala la lishe kwa watoto wao kwani sio wote wanaopata chakula shuleni, ufuatiliaji duni wa wazazi na walezi kwa maendeleo ya watoto wao pamoja na ukosefu wa bweni la shule.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Afisa elimu Sekondari Wilaya ya Misenyi ambaye pia ni mlezi wa shule ya Bugandika Pancras Ishengoma amewapongeza walimu hao kwa jitihada kitaaluma huku akiwaomba wazazi kuunga mkono juhudi za shule hiyo ili kufanikisha mipango ya kitaaluma ikiwa ni pamoja ikiwa ni pamoja nawazazi hao kuwakemea watoto wao kwenda disko za usiku, kumiliki simu wakiwa bado shuleni.

Ishengoma ameongeza kuwa atachukua wiki moja ya kuweka kambi shuleni hapo kwa ajili ya kuona nidhamu kwa watoto hao ili wafikie malengo yao huku akiwahimiza wazazi kutoa lishe ya watoto wao kwa wakati pamoja na kujenga utamaduni wa kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi pindi wanapokuwa wamefanya vizuri.

Kwa upande wake Afisa elimu kata Bugandika Marystella Stephano Kankiza amewaomba wazazi wa wanafunzi hao kuondokana na yaliyopita kipindi cha nyuma badala yake wasonge mbele ikiwa ni pamoja na kutowakatisha tamaa Walimu wa shule hiyo na kufanyia kazi mikakati iliyowekwa ili kuifanya shule hiyo kufaulu.

Aidha naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM katika kata ya Bugandika na katibu wa Mbunge Wilaya ya Misenyi Steven Elias  amewahimiza wazazi kuandaa Mazingira mazuri kwa watoto wao huku akiwaomba kuwatia moyo walimu ili wafanye kazi yao vizuri  na kuwa na mahusiano mazuri kwa walimu, kushirikiana vyema ili kujenga shule hiyo huku wakikazia suala la nidhamu ili kuwa na kizazi bora.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Bugandika Amudi Migeyo amesema ushirikiano wa pamoja kwa wazazi na walimu ndio utakaoivusha shule hiyo ambapo pia amwwasisitiza wazazi kutambua kazi nzuri inayofanywa na walimu hao pamoja na kutimiza wajibu wao pale inapopitishwa mipango ya shule pamoja na vikao mbali mbali vinavyolenga kujadili masuala mbali mbali ya shule.

Hata hiyo kwa upande wao wazazi wa wanafunzi hao akiwemo Jonimery Philimon, Mudhihir Uwesu Frednand  Felician wamewasisitiza wanafunzi hao kuwa na nidhamu ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi katika masomo ili kutimiza ndoto zao za baadae.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...