Saturday, February 8, 2025

CCM RUVUMA WAFANYA MKUTANO MKUBWA KUUNGA MKONO DKT. SAMIA, DKT. MWINYI KUPEWA MITANO TENA!!


Baadhi ya Wanachama wa CCM wakiwa katika matembezi ya kuunga mkono Azimio hilo la kuchaguliwa kuwa wagombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma.
Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Mkoa wa Ruvuma Hemed Challe akiongoza matembezi hayo ya kuunga mkono juhudi za kuwapongeza wagombea wa nafasi za Urais kupitia Chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akiongoza matembezi ya hiari katika juhudi za kuunga mkono wagombea wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye mkutano
Wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo
Na Regina Ndumbaro Ruvuma. 

 Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma kimefanya mkutano maalum wa kujadili na kupitisha azimio la kuwaunga mkono viongozi walioteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya urais kwa uchaguzi ujao. 

Mkutano huo, uliofanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, umeonyesha mshikamano mkubwa wa wanachama wa CCM mkoani humo katika kuimarisha chama kuelekea uchaguzi.


Katika azimio hilo, viongozi walioteuliwa kugombea nafasi ya urais ni Dkt. Ally Hassan Mwinyi kwa upande wa Zanzibar na Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgombea Mwenza Dkt. Emanuel Nchimbi kwa upande wa Tanzania Bara. 

Mwenyekiti Oddo Mwisho amewahimiza wanachama wa CCM mkoani Ruvuma kuwaunga mkono viongozi hao na kushiriki kikamilifu katika kampeni za chama kwa lengo la kuleta ushindi mnono katika uchaguzi huo.

Mbali na kujadili wagombea wa nafasi ya urais, mkutano huo pia ulijikita katika tathmini ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea mkoani Ruvuma chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Mradi mkubwa wa umeme na maji wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 400 umetajwa kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yanayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Ruvuma.

Mwisho amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za mitaa unaendelea kwa kasi, jambo linalothibitisha dhamira ya CCM ya kuboresha miundombinu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. 

Amesema kuwa hatua hizo ni matokeo ya jitihada za serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Ruvuma amewashukuru viongozi wa chama na serikali waliowezesha kufanikisha maazimio hayo huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, kwa kushiriki katika mkutano huo na kuunga mkono azimio la kuwaimarisha wagombea wa CCM katika uchaguzi ujao.

Pia amewapongeza madiwani na wabunge waCCM kwa mshikamano wao na juhudi zao za kushirikiana na wananchi katika kuimarisha chama na kutekeleza miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Ruvuma. 

Amesisitiza kuwa mshikamano huo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha CCM inaendelea kuwa chama kinacholeta maendeleo ya kweli kwa Watanzania.

Akihitimisha hotuba yake, Mwenyekiti Oddo Mwisho amewataka wanachama wa CCM Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ushindi wa chama hicho kwenye uchaguzi ujao. 

Amewasihi kushiriki kikamilifu katika kampeni na kuwahamasisha wananchi kuendelea kuiamini CCM kama chama chenye dira na maono ya maendeleo ya taifa.

Aidha wanachama wa CCM wameahidi kuendelea kuiunga mkono serikali ya CCM na viongozi walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao.

Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...