Tuesday, January 7, 2025

Mbowe "Nimemfadhili Sana Tundu Lissu Kwa Mfuko Wangu Mpaka Gari Nilimpa




"Unapokuwa huna shukran kwa mambo madogo madogo hata mambo makubwa huwezi kuwa nayo na shukran Nikupe stori yangu fupi na @tunduantiphaslissu Lissu mimi na Dkt. Silaa ndio tulimshawishi kuingia CHADEMA na wakati huo nafahamiana na Lissu alikuwa kwenye siasa kwenye uchaguzi wa mwaka 1995 akiwa na chama cha NCCR Mageuzi bahati mbaya matokeo yakatoka hakutangazwa mshindi baadae akaenda nafikiri masomoni akarudi nchini akafanya kazi nyingi za kiharakati na sheria na akawa ni mwanasheria aliyejitanabaisha kwamba ni mtu ambaye anatetea haki za watu wanaoonewa hasa migodini na vitu kama hivyo kipindi kile ndipo nilipokuwa karibu mimi na Lissu"

"Na akawa anakwenda kuwatetea wananchi wa Tarime kule kwenye migodi ya Nyamongo na maeneo mengine ya wachimbaji kipindi kile nikaanza kumdhamini yeye kama mwanasheria anayekwenda kuwatetea watu wanaoonewa. Kwa Lissu anakwenda kwenye kesi namlipia tiketi ya ndege mpaka Mwanza kwenda Musoma kutetea kesi wakati hata hayupo CHADEMA na kurudi Dar Es Salaam kwa mwezi kwa ofisi yangu binafsi sio chama."

"Mi nilikuwa kipindi hicho sio Kiongozi wa chama namgharamia namlipia ikafika mahalia baina ya 2004-05 akaingia CHADEMA nikamwambia kwa nini usigombanie ubunge akaniambia Mwenyekiti sijajiandaa safari hii nitagombea wakati ujao. Akaniambia Mwenyekiti naandaa Jimbo langu la uchaguzi Singida 'nisapoti' nikamuunga mkono kwa kumpa gari Nissan Patrol kaka nenda kajenge jimbo tulitaka uende bungeni 2010 kweli akaingia bungeni"

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa @chadematzofficial na Mtia nia wa nafasi hiyo Freeman Mbowe @freemanmbowetz akifanya mahojiano na Salim Kikeke @salim_kikeke mtangazaji wa Crown Media

Monday, January 6, 2025

VYANDARUA 1,542,836 VYENYE DAWA KUSAMBAZWA KATIKA MKOA WA SHINYANGA

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jumla ya vyandarua 1,542,836 vyenye dawa vinatarajiwa kusambazwa katika mkoa wa Shinyanga mwezi huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wake kupambana na ugonjwa wa malaria. 

Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 6,2025 wakati wa kikao kazi cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga juu ya kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa Mkoani Shinyanga.

Katika kikao hicho waandishi wa habari wamepitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo hali ya malaria nchini Tanzania na mkakati wa kinga dhidi ya malaria, kampeni ya ugawaji wa vyandarua mkoani Shinyanga, mbinu bora za kuwasilisha taarifa za malaria, taarifa muhimu kwa jamii juu ya kampeni ya ugawaji vyandarua na mchango wa vyombo vya habari katika utoaji wa taarifa za kampeni ya ugawaji vyandarua.

Vyandarua hivi vitasambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, huku lengo likiwa ni kupunguza maambukizi ya malaria.

Usambazaji huu utakuwa sehemu ya mpango wa kitaifa wa kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa Malari, ambao bado ni changamoto kubwa katika baadhi ya mikoa ya Tanzania.

Vyandarua vyenye dawa vimekuwa moja ya njia bora za kudhibiti maambukizi ya malaria. 

Serikali ya Tanzania inatarajia usambazaji huu utafikia kaya nyingi zaidi na hivyo kuokoa maisha ya wananchi. Usambazaji huu utafanyika kwa ushirikiano wa karibu na Serikali za Mitaa, na kwamba vyandarua vitasambazwa kwa usawa na kwa kasi ili watu wa maeneo ya vijijini wasiachwe nyuma.

Kwa sasa, wananchi wanahimizwa kutumia vyandarua vyenye dawa, na pia kuendelea kuchukua tahadhari nyingine kama vile kupiga dawa za kuua mbu katika makazi yao na kujiepusha na maeneo yenye maambukizi makubwa.



Sunday, January 5, 2025

Jackline Wolper Atangaza Rasmi Kuachana na Jack Wolper


Jackline Wolper ametangaza rasmi kwamba ameachana na mzazi mwenzake, Rich (Baba P), ambaye walifunga ndoa Novemba 19, 2022. Kupitia ujumbe aliouchapisha instagram, Wolper amewatoa wasiwasi mashabiki na marafiki zake waliokuwa wakimtumia jumbe za kumtia moyo na kumshauri kuhusu hali yake ya sasa.

Katika ujumbe wake, Wolper ameeleza kuwa yuko kwenye mchakato wa talaka rasmi na kwamba hana tena uhusiano wa kimapenzi na mzazi mwenzake. Ameomba mashabiki wake waache kumhusisha na mambo yanayoendelea upande wa Baba P, kwani sasa kila mmoja anaishi maisha yake kivyake.

"Licha ya changamoto za ndoa, tutabaki kuheshimiana kama wazazi na kuhakikisha watoto wetu wanalelewa katika mazingira mazuri," alisema Wolper.

Aidha, Wolper aliwashukuru wote waliomtumia jumbe za faraja na kusema kuwa anaendelea vizuri na maisha yake, akisisitiza kuwa furaha na amani ya moyo wake viko salama.

Saturday, January 4, 2025

Wananchi wa Arri Wanufaika na Mradi Mkubwa wa Maji



Na John Walter -Babati

Zaidi ya wananchi 3,000 wa Kata ya Arri, Wilaya ya Babati mkoani Manyara wameanza kunufaika na mradi mkubwa wa maji uliojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa ufadhili wa Shirika la Karim Foundation kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amezindua rasmi mradi huo leo januari 4,2025 na kuwapongeza wahisani kwa upendo wao na jitihada za kuchangia maendeleo ya jamii. 

Waziri Mkumbo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani, akisema miradi kama hiyo ni hatua kubwa kuelekea kufanikisha lengo hilo.

Mkurugenzi wa Karim Foundation Tanzania, Shau Erro Ae, ameeleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2.482 zimetumika katika mradi huo, huku wananchi wakichangia shilingi milioni 128 kwa nguvu kazi, ikiwemo kuchimba mitaro na shughuli nyingine za ujenzi. 

"Kwa sasa, hakuna mwananchi anayefuata maji umbali wa zaidi ya mita 400, hali ambayo imeboresha maisha ya wakazi wa Arri" alisema Shau

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, amesema mradi huo umeongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Babati Vijijini kufikia asilimia 83.

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo, amewashukuru wahisani na Serikali kwa jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji, akisisitiza kuwa mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa jamii ya Arri.

Wananchi wa Kata ya Arri wameeleza furaha yao kwa mradi huo, wakisema kuwa utapunguza changamoto za muda mrefu za upatikanaji wa maji safi na salama.

Mbunge Sillo aweka jiwe la msingi mradi wa maji Kata ya Arri.


Na John Walter -Babati

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Arri.

Mheshimiwa Sillo ameweka jiwe hilo la msingi leo Januari 3,2025, ambao unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usambazaji Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Babati, ukikadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 2.482.

Mfadhili mkuu wa mradi ni shirika la Karim Foundation, ambalo limechangia kiasi kikubwa cha fedha, huku wananchi wa eneo hilo wakichangia shilingi milioni 128.

Sillo amesema hayo ni matokea na matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kujenga mahusiano mazuri na sekta binafsi na mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, ameipongeza Karim Foundation kwa moyo wao wa upendo na msaada mkubwa kwa wakazi wa Babati. 

Amebainisha kuwa mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama mkoani Manyara, ambapo kwa sasa vijijini ni asilimia 71 na mijini asilimia 83.

Mradi huo ambao kwa sasa umeanza kutoa maji, unahudumia vijiji saba vilivyoko katika Kata ya Arri, na hivyo kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.

Mkurugenzi wa Karim Foundation Tanzania, Shau Erro Ae, amesisitiza dhamira ya shirika hilo kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi.

Wananchi wa Kata ya Arri walimshukuru Mheshimiwa Daniel Sillo na Karim Foundation kwa juhudi zao, wakisema mradi huo wa maji utakuwa suluhisho la changamoto kubwa waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa muda mrefu.

Aidha walionyesha shukrani zao kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa mradi huo utaboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.


HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI JANUARI 4, 2024

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...