Saturday, December 21, 2024

UZINDUZI WA NYUMBA 109 KWA WAATHIRIKA WA MAPOROMOKO YA TOPE MKOANI MANYARA


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Ndugu John Mongella, leo Desemba 20, 2024, amemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika hafla ya uzinduzi wa nyumba 109 zilizojengwa kwa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 3 Desemba 2023, mkoani Manyara.

Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Mongella ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo unakamilika kwa wakati. Alisema hatua hiyo ni kielelezo thabiti cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayolenga kuimarisha ustawi wa jamii na kuboresha maisha ya wananchi.

"Tunajivunia kazi kubwa inayotekelezwa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Chama Cha Mapinduzi wakati wote kitakuwa karibu na Serikali katika juhudi zote za kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi," alisema Mongella.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amepongeza Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake kwa kushirikiana na serikali wakati wa zoezi la uokoaji na katika hatua za kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo.

"Tunatoa shukrani za dhati kwa CCM kwa msaada wao mkubwa katika mchakato wa kusaidia waathirika, ikiwemo rasilimali na nguvu kazi. Nyumba hizi ni ushuhuda wa mshikamano wetu wa kitaifa katika kukabiliana na changamoto za majanga," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Nyumba hizi 109, zilizojengwa kwa ustadi na kwa kuzingatia mahitaji ya waathirika, zimekuwa alama ya matumaini mapya kwa familia zilizoathirika. Uzinduzi huu ni hatua muhimu ya kuwawezesha waathirika kuanza maisha upya kwa heshima na usalama, huku ukidhihirisha dhamira ya serikali na CCM ya kuwaletea maendeleo wananchi wote.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...