Na John Walter -Manyara
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetangaza mpango wa kusambaza mitungi 16,275 ya gesi ya ujazo wa kilo sita kwa kila mwananchi mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya watumiaji ifikapo mwaka 2034.
Awali Mpango huo ulianza kwa kishirikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Magereza, na shule mbalimbali.
Mkurugenzi wa Teknolojia Jadidifu na Nishati Mbadala kutoka REA Mhandisi Advera Mwijage amesema mitungi hiyo 16,275 itasambazwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 284 kati ya jumla ya shilingi bilioni 8.6 zilizotengwa kitaifa kusambaza gesi kwa wananchi kwa bei ya ruzuku.
Mhandisi Advera amesema kwa mkoa wa Manyara mtungi mmoja wa ujazo wa kilo 6 utauzwa kwa bei ya shilingi 17,500 badala ya bei ya awali ya shilingi 35,000 kwa kila mtungi wa ujazo wa kilo sita.
Amesema Kampuni ya Manjis imepewa jukumu la kusambaza mitungi hiyo kwa gharama ya Shilingi 35,000 kwa kila mtungi ambapo serikali italipa asilimia 50 ya bei hivyo mwananchi atanunua kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 kama ilivyodhamiria Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Advera pia ametangaza fursa ya mikopo ya masharti nafuu ya hadi shilingi milioni 120 kwa wanaotaka kufungua biashara ya vituo vya kuuzia mafuta maeneo ya vijijini kwa lengo la kusogeza nishati hiyo karibu na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amepongeza jitihada hizo za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Manyara kuchangamkia fursa hiyo kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kuboresha afya na mazingira.
Amesema mpango huo unalenga kuleta mabadiliko makubwa katika matumizi ya nishati safi nchini, huku ukihakikisha upatikanaji wa gesi kwa gharama nafuu kwa wananchi wa kawaida.