Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Wakili Stephen Byabato, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamewakutanisha watoto yatima 200 wanaoishi katika vituo vya watoto yatima Manispaa ya Bukoba. Lengo kuu ikiwa ni kuwapa faraja kwa kuwapa mahitaji muhimu ya shule, vyakula na mahitaji binafsi ikiwa ni sadaka na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa wadau hawa kuelekea mwisho wa mwaka 2024.
Tamasha hilo limefanyika tarehe 14/12/2024 kwa jitihada za wadau waliopo katika Kundi Songezi (WhatsApp Group) la Bukoba Mjini Mpya chini ya ulezi wa Mhe. Byabato na wadau nje ya kundi hilo.
Katika maandalizi ya tamasha hilo, zaidi ya Tsh 10 Milioni zilitolewa na wadau na leo wamekabidhi sadaka mbalimbali kwa watoto yatima zikiambatana na tuzo za utambuzi kwa waanzilishi na vyeti vya shukrani kwa wasimamizi wa vituo hivyo kwa kazi kubwa ya kuijenga Jamii bora ya Bukoba.
Pamoja na zawadi nyingi zilizotolewa (zikiwemo za sikukuu), vimetolewa vitabu vya dini (Biblia na Quran Takatifu) yametolewa madawati 50 kwa shule za msingi zenye uhitaji zaidi za Byabato, Bilele, Rwamishenye na Bunena.
Aidha katika kuunga jitihada za Mbunge Byabato, Mdau kutoka Afrika Kusini, Injinia Datusi, ametoa vitanda 20 kwa watoto yatima, huku wafanyabiashara wa Soko Kuu Bukoba na wadau wengine wakitoa zawadi mbalimbali kwa watoto hao, TRA Kagera wakakamilisha furaha kwa kuwalisha wahudhuriaji wote zaidi ya 500 chakula cha pamoja cha kiwango cha juu.
Mbunge Byabato kakamilisha Tamasha hili kwa kuwaalika wana Bukoba wote katika Tamasha kubwa la Mkoa wa Kagera chini ya uanzilishi na usimamizi wa Mhe. Mkuu wa Mkoa Bi. Hajjat Fatma A. Mwassa kuanzia jumatatu ya tarehe 16/12/2024.
Wadau mbalimbali wamepongeza ubunifu, mafanikio na majitoleo hayo yaliyoratibiwa vema na Kamati ya Maandalizi. Wameomba tamasha hili liwe endelevu kwa ajili ya kuwaleta pamoja watu wote.
Source