Thursday, December 12, 2024

GDSS YALETA MAFANIKIO CHANYA DHIDI YA VITENDO VYA UKATILI 2024


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WANAHARAKATI kupitia Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii hasa katika kuhakikisha mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla wanapata haki zao za msingi pamoja na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia.

Akizungumza jana Desemba 12, 2024 wakati wa Semina za Jinsia na Maendeleo ambazo hufanyika kila Jumatano katika viwanja vya TGNP Mtandao Jijini Dar es Salaam, Mwanaharakati kutoka Mabibo, Bw. Venance Peter amesema kupitia semina hizo wameweza kujengewa uwezo na kuwa sehemu ya kuelimisha jamii na kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikitokea kwenye jamii zao ikiwemo kumlinda mwanamke na mtoto dhidi ya ukatili.

Amesema wamekuwa ni sehemu ya mabadiliko katika jamii hasa katika kuelimisha makundi rika kupitia Gender Club za mashuleni na kuweza kupunguza vitendo vya ukatili mashuleni na kwenye jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwanaharakati kutoka Mbezi Beach, Bi. Flora Baltazary amesema kupitia semina hizo wananchi wameweza kupata hamasa zaidi kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na wanwake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi.

"Kwenye semina hizi hamasa zilitokea huku, wanawake kuwaambia wanaweza na wanaweza kweli kwani tumeona sehemu nyingi wameweza kugombea kitu ambacho ni matokeo wanaGDSS kwa mwaka huu 2024". Amesema

Aidha amesema wamekuwa wakipaza sauti dhidi ya ukatili ambao ulikuwa ukiendelea na kuweza kuleta matokeo chanya kwa wahusika kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua stahiki.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...