Thursday, November 21, 2024

WENYE MATATIZO YA KIAFYA KUPEWA KIPAUMBELE KUPIGA KURA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah   
Na Hadija Bagasha Tanga, 

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amewataka viongozi wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha watu wenye matatizo ya kiafya, ambao hawana uwezo wa kufika vituoni kupiga kura, wanapatiwa usafiri ili kuhakikisha kila mtu anashiriki zoezi hilo kikamilifu. 

Hatua hii inalenga kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa maendeleo ya nchi yao.

Pia Serikali imewatoa hofu wananchi kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa kuwa utafanyika Kwa salama na amani na atakae jaribu kuleta chokochoko atachukuliwa hatua Kali za kisheria.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu mlezi wa chama hicho , Hemed Suleiman amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi wote katika uchaguzi huo huku  akiungwa mkono na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abrahman Abdallah. 

"Kwenye hili lazima wapo viongozi wakae mbele kuona kila eneo kila nyuma kuangalia nani ameenda kupiga kura na ambaye hajakwenda kujua sababu gani pengine afya yake sio nzuri apelekewe usafiri aende kupiga kura tusikubali tukamwacha mtu yeyote bila kupiga kura niwahakikishie nchi yetu itaendelea kuwa salama kura zitapigwa kwa amani kabisa,"alisisitiza Makamu wa pili wa Rais.

Alisema kuwa serikali imejipanga kuimarisha usalama na amani Ili wananchi waweze kushiriki vizuri katika uchaguzi na kuendelea na majukumu yao.

"Watanzania niwaondoe wasiwasi uchaguzi huu ni salama ila niwaonye wale ambao wanania ya kuuharibu basi hatutasita kuwachukulia hatua"alisema Makamu wa Rais 

Aidha alivitaka vyama kuendesha kampeni za amani bila ya vurugu wala matusi kwani sifa za watanzanzia ni kudumisha amani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abrahman alisema kuwa katika ya vijiji 763 wapinzani wamesimamisha wagombea katika vijiji 140 pekee hivyo hiyo inatupa matumaini ya kushinda Kwa kishindo katika uchaguzi huu.

Aidha, baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo walionyesha msisitizo wa kushiriki kwenye uchaguzi kwa kusema kuwa ni fursa ya kuchangia maendeleo ya taifa.

Ushiriki wa wananchi wote, bila kujali hali zao za kiafya au mazingira, ni muhimu kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na jumuishi, Viongozi wa mkoa wanatakiwa kutekeleza jukumu lao la kuwezesha usafiri kwa wale walio na changamoto ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza haki yake ya kikatiba.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...