Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Fernidand Makore, amesema kwa mujibu wa sheria za Tanzania, taratibu za ukamataji zinamtaka Polisi akienda kumkamata Mtuhumiwa kwanza ajitambulishe na aonesha hati ya ukamataji (arrest warrant) akiwa na gari la Polisi linalotambulika hivyo waliohusika kwenye tukio la Mfanyabiashara Deogratius Tarimo wawe ni Polisi au Watu wengine wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwakuwa wamekiuka sheria.
"Hii ya kukamata holela ndio inatengeneza makosa ya utekaji ambayo ni ya jinai, maoni yangu Mtu akija hajajitambulisha usikubali akukamate, akija Mtu na silaha kwa kutumia nguvu kama Tarimo alichofanya hapa ni kujitetea mwenyewe (self defence), kwa mujibu wa sheria kuna utetezi binafsi, kwahiyo Mtu akija kukukamata na hajajitambulisha jitetee hata ukienda Mahakamani ukiwa na kosa utasema nilikuwa najitetea kulinda usalama wangu binafsi" ameeleza Wakili Makole
Baada ya tukio hili la kutaka kutekwa kwa Mfanyabiashara Deogratius Tarimo, Mawakili/Wanasheria mbalimbali wa Tanzania wamejitokeza kuikumbusha jamii ya Watanzania sheria inasemaje pale wanapofuatwa kukamatwa na Polisi ambapo Wakili Jebra Kambole ameandika yafuatayo.
Usikubali kukamatwa na Mtu;
1. Kavaa kiraia
2. Gari halina namba au namba za kiraia
3. Watu ambao hawajatoa vitambulisho
4. Watu wasiokwambia kosa lako na kwamba uko chini ya ulinzi.
5. Watu wasio na hati ya ukamataji!!