Tuesday, October 29, 2024

Mradi wa Sh 60 bilioni kuleta mapinduzi ya huduma za usafiri Ziwa Victoria


Mwanza

 Serikali ya Tanzania imewekeza Sh 60 bilioni kuboresha bandari tatu kuu za Ziwa Victoria.

Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Erasto Lugenge aliwaambia wandishi wa habari waliotembelea bandari za Bukoba na Kemondo kuwa uwekezaji huu mkubwa katika bandari za Kemondo, Bukoba na Mwanza Kaskazini unatarajiwa kuboresha ufanisi na uwezo wa huduma za usafiri katika eneo hilo.

Bw. Lugenge, ambaye anasimamia bandari 12 upande wa Tanzania wa ziwa hilo, amesema kuwa kazi inaendelea vizuri, huku Bandari ya Kemondo ikiwa karibu kukamilika.

"Kazi ya kuboresha Bandari ya Kemondo, ambayo imepewa uwekezaji wa Sh20.339 bilioni, imekamilika kwa asilimia 98," alisema, akiongeza kuwa hatua za mwisho zinahusisha kusafisha eneo kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Mradi wa kuboresha Bandari ya Bukoba kwa Sh19.544 bilioni umefikia asilimia 75 ya kukamilika.

"Kwa mujibu wa makubaliano, miradi hii ilikuwa imepangwa kukamilika ndani ya miezi 18, ikitarajiwa kukamilika tarehe 4 Novemba 2024. Kwa kuwa kazi nyingi tayari imefanyika, sasa ni juu ya mkandarasi na mhandisi mshauri kutathmini kama itakamilika kwa wakati au kama itahitajika muda mfupi kidogo ili kumaizia," Bw Lugenge alisema.

Miongoni mwa bandari 12 anazosimamia Bw. Lugenge, sita ni vituo vikuu, vikiwemo Mwanza Kaskazini, Mwanza Kusini, Bukoba, Kemondo, Nansio-Ukerewe, na Musoma. Maboresho yanayoendelea yanakusudia kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 hadi mita 5 katika Bandari za Kemondo na Bukoba. Pia, mabadiliko mengine yanahusisha kuongeza urefu wa gati kutoka mita 75 hadi 92, kuboresha eneo la sakafu kwa kuimarisha muundo wa zege, na kufunga uzio wa kuimarisha usalama.

Maboresho mengine yanajumuisha ujenzi wa maeneo ya kusubiri abiria, vituo vya ukaguzi wa mizigo, mfumo wa umeme wa kisasa, na kinga ya upepo.

"Tunaanzisha vituo vya huduma vya sehemu moja katika bandari zote zinazoboreshwa, tukijumuisha huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Misitu, Uhamiaji, Afya, na Wakala wa Forodha na Uondoshaji Mizigo pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama ili kuboresha utoaji wa huduma," Bw Lugenge alieleza.

Maboresho haya yanalenga kusaidia kupokea MV Mwanza Hapa Kazi Tu, meli mpya ya abiria inayojengwa na ambayo itakuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki. MV Mwanza Hapa Kazi Tu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20, na magari makubwa matatu, hivyo kuongeza maradufu uwezo wa abiria ikilinganishwa na MV Victoria inayobeba abiria 600 kwa sasa.

Meli hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake Desemba 2024 au Januari 2025, na maboresho ya bandari yanapiga hatua ili kukidhi muda wa uzinduzi. "Tunatarajia kuwa MV Mwanza Hapa Kazi Tu itaanza kufanya kazi mwishoni mwa mwaka au mwanzoni mwa mwaka ujao, hatua ambayo italeta maboresho makubwa katika huduma za usafiri kwenye Ziwa Victoria," Bw Lugenge alithibitisha.
Uwekezaji wa serikali na kukamilika kwa maboresho haya ya bandari yanatarajiwa kurahisisha safari na kuongeza shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, na kuweka viwango vipya kwa huduma za usafiri wa ziwani kote Afrika Mashariki.

Tayari nchi za Burundi, DRC na Rwanda zimeonyesha nia ya kutumia bandari hizo zitakapokamilika.

Hili litawezekana kutokana na uwepo wa huduma ya reli ya kisasa ya SGR na reli ya MGR, zinazounganisha Jiji la Dar es Salaam na Ziwa Victoria kupitia Mwanza.

NECTA yatangaza matokeo ya Darasa la Saba 2024, yatazame hapa

 




NECTA yatangaza matokeo ya Darasa la Saba 2024, yatazame hapa

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani ya darasa la saba mwaka 2024 huku ufaulu wa jumla ukiongezeka kwa asilimia 0.29 kulinganisha na mwaka 2023.


Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 29, 2024 jijini Dar es Salaam amesema ufaulu wa jumla umeongezeka kutoka asilimia 80.58 iliyorekodiwa mwaka 2023 hadi asilimia 80.87 mwaka huu.


"Watahiniwa 974,229 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C, Aidha takwimu zinaonesha kuwa ufaulu katika masomo yote sita yaliyotahiniwa umeendelea kuimarika,"amsesema Dk Mohamed.


Septemba 2024 jumla ya watahiniwa wa darasa la saba 1,204,899 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi sawa na asilimia 98 kati ya watahiniwa 1,230,774 waliosajiliwa kufanya mtihani huo.


Kati ya watahiniwa hao waliofaulu mtihani huo taarifa ya Necta inabainisha kuwa wavulana walikuwa 449,057 sawa na 46 na wasichana 525,172 sawana 54.


Aidha, Dk Mohamed amebainisha kuwa kuna uwiano sawa wa ufaulu kwa wasichana na wavulana katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka huu.


"Ubora wa ufaulu umeimarika kwa jinsi zote kwani kwa wasichana kuna ongezeko la asilimia 9 na kufikia asilimia 33 na wavulana kuna ongezeko la asilimia 8 na kufikia asilimia 39 kulinganisha na mwaka jana," ameongeza Dk Mohamed.


Nekta inafafanua zaidi uwiano huo wa ufaulu umeonekana pia katika ubora wa ufaulu wa daraja A na B ambapo kati ya watahiniwa 431,689 waliopata madaraja hayo wasichana ni 216,568 sawa na 50.1 na wavulana ni 215,121 sawa na asilimia 49.9.

NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA - PSLE-2024 EXAMINATION RESULTS

Habari kubwa za Magazeti ya Tanzania leo October 29, 2024

 Good Morning Mtu wangu wa nguvu kutoka Dar es salaam October 29, 2024,nakukaribisha kutazama kile kilichoandikwa katika kurasa za mbele na za nyuma za Magazeti ya Tanzania.

              

The post Habari kubwa za Magazeti ya Tanzania leo October 29, 2024 first appeared on Millard Ayo.

Kipa Emiliano Martinez Ashinda Tena Golikipa Bora wa Dunia....




Golikipa wa klabu ya Aston Villa raia wa Argentina, Emiliano Martinez (32) ameshinda tena tuzo ya Golikipa bora wa Dunia katika sherehe za ugawaji wa tuzo hizo nchini Ufaransa.

Martinez ambaye amekuwa sehemu ya kikosi cha Aston Villa kilichomaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Uingereza 2023/24 pamoja na golikipa tegemezi wa Argentina katika kikosi kilichoshinda michuano ya Copa America 2024 ameshinda tuzo hiyo inayojulikana kama 'Yashin Trophy' kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushinda kwa mara ya kwanza mwaka 2023.

Martinez ameshinda tuzo hiyo kwa kuwashinda wapinzani wake kama Unai Simón (27) anaedakia klabu ya Athletic Bilbao ya Uhispania na Timu ya Taifa ya Hispania ambapo aliisaida timu yale kushinda ubingwa wa michuano ya UEFA Euro, pia Martinez amembwaga golikipa wa Dortmund na Timu ya Taifa ya Uswizi, Gregor Kobel (26) ambaye alifanya vizuri na klabu yake licha ya kupoteza katika mchezo wa fainali la Ligi ya Mabigwa dhidi ya Real Madrid.

Monday, October 28, 2024

CCM KATA YA KISHAPU YAMALIZANA NA FOMU ZA SERIKALI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Maandamano yaliyoanzia viwanja vya Shirecu,ofisi ya mtendaji kata ya  Kishapu kisha kumalizikia ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga ambapo wagombea nafasi za uenyeviti wa mitaa Kata ya Kishapu wakienda kuchukua fomu ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa serikali yakiongozwa na mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kishapu Janipher Juma - Picha na Sumai Salum
Mwenyekiti Mpya wa UVCCM Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga aliyechaguliwa Jana na wanachama wa Chama hicho Jeniphe  Juma akizungumza Leo Oktoba 28 ,2024  na wanaCCM kwenye viwanja vya ofisi ya Msimamizi wa uchaguzi Kata ya Kishapu kwenye tukio la uchukuaji fomu za kugombea serikali za Mtaa.
Baadhi ya wagombea nafasi ya uenyeviti wa mitaa kupitia Chama cha Mapinduzi CCM katika Kata ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakionesha fomu za uchaguzi kwa wanachama wa Chama hicho baada ya kuchukua,kujaza kisha kurudisha  nje ya ofisi ya mtendaji wa kata hiyo.

Na Sumai Salum - Kishapu

Wagombea saba  nafasi ya Mwenyekiti wa serikali za mitaa kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wamechukua fomu za serikali za kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.

Zoezi hilo limefanyika Leo Oktoba 28,2024 likiambatana na maandamano ya kutembea kwa miguu kuanzia viwanja vya Shirecu kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi kisha kumalizikia katika viwanja vya ofisi ya Ccm Wilaya huku mwenyekiti mpya wa UVCCM Jenipher Juma  na Diwani wa Kata hiyo Mhe. Joel Ndettoson wakiongoza maandamano hayo na 

Akizungumza baada ya uchukuaji fomu hizo  mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kishapu Jenipher Juma amewataka wagombea na wanaCCM wote kuendelea kuwa watulivu wakingojea muda wa kampeni huku wakiendelea kuonesha umoja kama walivyoonesha kwa kuwasindikiza.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kishapu Mhe. Joel Ndettoson amewapongeza wagombea wote walioshiriki kugombea ndani ya Chama na kisha kupatikana baadhi watakaopeperusha bendera ya Chama hicho kuwa hayo yote ni maamuzi ya wanachama wenyewe wanachotakiwa kufanya ni kushirikiana,kuungana,kupendana na kusaidiana.

"Ndugu zangu Leo hii tunashuhudia ndugu zetu wagombea wamechukua fomu,wamejaza na kisha wamerudisha hivyo hapo baadae tutawafahamisha tarehe ya kuzindua zoezi zima la kampeni lakini tuonyeshe uzalendo kwa jamii huku tukielewesha umuhimu wa kupiga kura katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa" ,ameongeza Ndettoson 

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Kishapu Godwin Everygist amesema kuwa zoezi la uchukuaji fomu za serikali litasitishwa mnamo tarehe 1 Novemba  saa kumi kamili (1:00)  jioni hivyo vyama vyote vya siasa vinavyogombea vihakikishe vinapeleka wagombea kuchukua fomu na kujaza kisha kurejesha kabla ya muda kuisha.

 Wagombea Saba (7)  waliotoka vitongoji Saba vinavyounda  Kata ya Kishapu ni pamoja  na Kitongoji cha Mwasele "B",Lugaba,Lyandu,Mhunze,Kishapu,Isoso pamoja na Mwabusiga na wote wamechukua fomu wamejaza na kisha wamerudisha.
Maandamano yaliyoanzia viwanja vya Shirecu,ofisi ya mtendaji kata ya  Kishapu kisha kumalizikia ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga ambapo wagombea nafasi za uenyeviti wa mitaa Kata ya Kishapu wakienda kuchukua fomu ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa serikali yakiongozwa na mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kishapu Janipher Juma 
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Lubaga) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw.Mahona Makaranga(kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia)
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Mwasele B) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw.Fabian Juma Makongo(kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia) 
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Isoso) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw.Robert Nyahuma (kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia) 
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Mwabusiga) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw. Charles Bugangali(kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia)
Mgombea uenyekiti wa mtaa wa Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw. Meshack Kuyenza (kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw. Godwin Evsrygist(kulia) Leo Oktoba 28,2024
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Mhunze) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw.Hamadi Said Khalfan(kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia)
Mgombea uenyekiti wa mtaa (Lyandu) Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha  Mapinduzi CCM Bw.Joseph Mabula(kushoto) akikabidhi fomu ya ugombea kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Kishapu Bw.Godwin Evsrygist(kulia)

Katibu wa CCM Kata ya Kishapu Wilayani Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Bw. Cornel Zengo akizungumza Leo Oktoba 28,2024 kwenye zoezi la wagombea wa serikali za mitaa kuchukua fomu za serikali Wilayani humo.

Sunday, October 27, 2024

Elimu ya Mpiga Kura Yazidi Kuimarishwa Katika Maeneo ya Vijijini Tanzania


Na Mwandishi Wetu

Ngorongoro, Oktoba 27, 2024 – Katika juhudi za kuhakikisha ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi unaongezeka, mradi wa #MpigaKura255 unaoratibiwa na mashirika ya Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation umeendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa wakazi wa maeneo ya vijijini, ukiwalenga hasa wale wa jamii za pembezoni. 

Lengo kuu la mradi huu ni kuwapa wananchi uelewa wa haki na wajibu wao ili waweze kufanya maamuzi sahihi na yenye mantiki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.

Ezekiel Ndotunti, mmoja wa watoa elimu kutoka mradi wa #MpigaKura255, ameendelea na zoezi la kutoa elimu katika kitongoji cha Maasusu, kata ya Pinyinyi, kijiji cha Pinyinyi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Ndotunti amesisitiza kuwa elimu hii inawapa wananchi nafasi ya kuwa na sauti katika kuchagua viongozi wanaoweza kuwawakilisha kwa usahihi, akiwataka waone kuwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ni haki na wajibu wa kila mmoja kwa maslahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Efrem Genge, mtoa elimu ya mpiga kura kutoka kata ya Oldonyo Sambu ambaye amepitia mafunzo maalum kutoka Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, alikuwa na haya ya kusema: "Leo, tarehe 26 Oktoba 2024, nimeendelea na zoezi la kutoa elimu ya mpiga kura katika kijiji cha Jema, na nimeweza kuwafikishia ujumbe huu kwa wapiga kura 58, ambapo wanawake walikuwa 27 na wanaume 31." Genge alieleza kuwa elimu anayotoa inalenga kuwaandaa wananchi kwa ajili ya kufanya maamuzi yanayojenga jamii imara na yenye mwelekeo wa maendeleo.

Naye Sarah Laizer Mtoa Elimu ya Mpiga kura aliyewezeshwa na asasi za Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation kutoka Kata ya Engoserosambu katika tarafa ya Sale alikuwa na haya ya kueleza "nilijengewa uwezo wa kutoa Elimu ya Mpiga kura ijumaa tarehe 25 Oktoba 2024, na haraka sana siku iliyofuata tarehe 26 Oktoba 2024 Jumamosi nilirudi kwenye kata yangu na kuanza kutoa Elimu ya Mpiga kura kwenye Kijiji cha Orkiu Juu, na kwa muda mfupi tu nimefikia wananchi 384, kati ya hao wanawake walikuwa 213 na wanaume 171. Dhamira yangu ni kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa siku tano zijazo"

Mradi wa #MpigaKura255 unalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anajua na kuelewa thamani ya kura yake, huku ukisisitiza kwamba nguvu ya mabadiliko na ujenzi wa taifa la kidemokrasia iko mikononi mwa wananchi wenyewe. Kwa kutoa elimu kwa jamii za vijijini kama katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mradi huu unapania kuleta usawa na haki kwa wananchi wote kwa kujenga jamii iliyo na mwamko wa kidemokrasia na kuwajibika kwa kutumia kura kwa uangalifu na hekima.

Kupitia elimu hii, wananchi wa Ngorongoro wanapewa fursa ya kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ya kidemokrasia kwa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Zozi hili linaendana na kaulimbiu ya #MpigaKura255 na #Pigapigika, ikisisitiza kuwa ushiriki wa kila mmoja ni muhimu katika kujenga taifa bora lenye misingi ya uwazi na uwajibikaji. Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, kupitia mradi huu, zimedhamiria kukuza demokrasia nchini Tanzania na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata nafasi sawa ya kushiriki katika michakato ya uamuzi wa kitaifa kwa ajili ya mustakabali bora wa nchi.







Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...