Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kupanua wigo wa uwekezaji nje ya mipaka ya nchi. Hayo yameelezwa wakati wa kikao kazi cha siku tatu kinachohitimishwa hivi leo jijini Arusha.
Kikao hicho kilichofunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan na kuwakutanisha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kujadiliana mikakati mbalimbali ya mageuzi ndani ya taasisi za umma na uwekezaji wenye tija.
Kauli mbiu ya kikao kazi hicho "Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Nje ya Tanzania" inagusia namna ambavyo taasisi na mashirika ya umma yanaweza kupanua wigo nje ya soko la ndani.
Kauli mbiu hii ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais katika kikao kazi kama hicho kilichofanyika mwaka jana, kuwataka wakuu wa taasisi za umma kutafuta fursa za kimataifa. Kikao hiki kimetoa fursa nzuri kwa wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi za umma kutathimini maboresho waliyofanya toka kikao kilichopita na kuainisha mikakati mipya ya mipango ijayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Adam Mihayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB alisema, "Ili kufanikiwa nje ya mipaka ya Tanzania, ni lazima tulitambue soko lengwa kwa kufanya tafiti za kina ili kubaini mianya ya fursa na kutengeneza bidhaa na huduma zetu kadri ya mahitaji ya soko la kimataifa."
Alisisitiza pia umuhimu wa mashirika hayo kuunda ubia wa kimkakati, ushirikiano, na muungano ili kutumia mtandao wao wa ndani na utaalamu. Aliongeza kuwa, "Muundo wetu wa kibiashara unatakiwa uwe wa kibunifu na wenye uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira, ili kukabiliana na mahitaji tofauti tofauti ambayo ni muhimu ili kufanikiwa katika soko la kimataifa."
Mihayo aliendelea kufafanua kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za umma. "Ni muhimu kutumia uwezo wa mashirika yetu kufanya kazi tukiungana pamoja kwa kushirikishana takwimu, kupanga mikakati pamoja, na kusadiana katika utoaji wa huduma.
Kwa kufanya hivyo, tutaboresha rasilimali zetu na pia tutawapa wateja wetu huduma bora kulingana na mahitaji yao na kujenga imani yao kwetu." Alibainisha kuwa ushirikiano wa kimkakati katika tafiti na kubadilishana takwimu baina ya taasisi zinazotegemeana zinaweza kuwasaidia kufikia malengo yao na kuzifanya taasisi hizo kufanya vizuri sokoni.
Akielezea utekelezaji uliofanywa na Benki ya TCB, Mihayo aliwaelezea washiriki mafanikio ya hivi karibuni ya benki hiyo ikiwemo uzinduzi nchini Comoro wa huduma za kibenki kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora Banking).
"Hii inaonyesha dhamira yetu ya kutoa huduma za kibenki nje ya mipaka na kuyafikia mahitaji ya
Watanzania wote dunia nzima. Katika dhamira hii, tunatarajia kuwa katika miaka miwili jayo tutaipeleka TCB katika Soko la Hisa (Dar es Salaam Stock Exchange), hivyo kumpa kila Mtanzania fursa ya kumiliki hisa na kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hii," alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Mihayo alitoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kutobweteka na soko la ndani, bali kuiga mfano wa mataifa yaliyofanikiwa kujipenyeza nchini mwetu na kuanzisha biashara zinazostawi. "Wametuonyesha kwamba inawezekana kufanya hivyo, ni wakati wetu sasa kuthubutu na kutumia fursa hii.
Tushirikiane pamoja, tuwe wabunifu, na kupanga mikakati pamoja ili kuhakikisha kwamba taasisi na mashirika ya umma yanajitegemea, yanachangia pato la taifa lakini pia yanakuwa mojawapo kati ya mashirika makubwa duniani."