Na Mwandishi Wetu
Serikali imeitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhakikisha inazingatia vigezo vilivyowekwa kisheria katika usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ili kuepuka kuwapatia watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa mapema leo Agosti 3, 2024 Jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo wakati akizungumza na watumishi wa vyombo vya usalama vilivyopo chini ya Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uangalizi pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
"Msigawe Vitambulisho vya Taifa bila kuzingatia vigezo vilivyoweka kisheria, hivi ni usalama wa nchi yetu, hakikisheni mnazingatia vigezo kwa wale wanaostahili Vitambulisho hivyo wanavipata kwa ajili ya matumizi mbalimbali" Amesema Naibu Waziri Sillo.
Aidha Naibu Waziri Sillo amesema hadi kufikia Agosti, 2024 Watanzania zaidi ya Milioni 24 wamesajiliwa katika mfumo wa NIDA huku zaidi Vitambulisho Milioni 21 tayari vimezalishwa kupitia Mamlaka hiyo na kati ya hivyo Vitambulisho Milioni 20 vimesambazwa kwa Wananchi.
Kuhusu usambazaji wa Vitambulisho hivyo Naibu Waziri Sillo ameziagiza Mamlaka hiyo kuhakikisha zinashusha kadi zote ambazo zimekamilika hadi ngazi za Vijiji ili Wananchi wazipate kwa urahisi.
"Kwa zile kadi ambazo zipo kwenye maeneo yetu, shusheni chini kwenye Kata na Vijiji ili Wananchi wapate Vitambulisho vyao vya Taifa ambavyo vimekamilika kwa ajili ya matumizi kwenye huduma mbalimbali zinazotolewa hapa nchini"Ameema Naibu Waziri Sillo.
Katika ziara yake ya siku mbili Mkoani Mwanza, Naibu Waziri Sillo, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa vituo vya Polisi vinavyojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwa ni pamoja na kituo cha Polisi cha Nyegezi Wilayani Nyamagana, Nyamohongolo kilichopo Ilemela na Zahanati ya Polisi Mabatini.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna Msaidi wa Polisi (DCP), Wilbrod Mutafungwa, ameipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuendelea kuwaongezea masilahi watumishi na watahakikisha wanatekeleza maagizo ya Serikali aliyotoa Mhe. Naibu Waziri wakati wa ziara yake.
"Mhe. Naibu Waziri nikuhakikishie kuwa tutaendelea kusimamamia nidhamu kwa swala zima la uadilifu hasa katika eneo la kutojihusisha kabisa na vitendo vya rushwa na tutawaelekeza zaidi wale waliopo chini yetu"Amesema DCP Mutafungwa.