MSANII Rajab Kahali, maarufu kwa jina la Harmonize, mmiliki wa Kundi la Konde Music kwa mara ya kwanza ameeleza ndoto yake ya kile anachopanga kukifanya baada ya kustaafu kazi yake ya muziki.
Katika mahojiano, msanii huyo alieleza kuwa anafahamu kabisa kuwa hatakuwepo kwenye tasnia ya muziki milele na tayari amebainisha ni kitu gani ataridhika nacho pindi taaluma yake ya muziki itakaposhuka.
Harmonize ambaye alisherehekea miaka yake 30 miezi michache iliyopita, alifichua ndoto yake ya kuwa daktari ili kuokoa maisha. Alieleza nia yake ya kusomea udaktari baada ya kustaafu muziki akiwa na miaka 45 hadi 50.
"Nimewaza huko mbeleni kazi yangu ya muziki ikishuka labda nikiwa na umri wa miaka 45-50 nitafikiria kusomea udaktari, angalau mwaka mzima ningependa kufanya kazi hospitalini ili kusaidia watu," Harmonize alisema.
Msanii huyo alieleza kuwa mbali na lengo lake la kutoa misaada ya kibinadamu kwa kuwatibu wagonjwa, pia anataka kuona furaha kwenye nyuso za watu kutokana na fani hii anayofikiria kuifanya licha ya kuishia darasa la saba.