Friday, August 13, 2021

Kina Mbowe waigeuzia kibao Serikali, Hakimu atoa agizo



Freeman Mbowe akiwa mahakamani Kisutu
KIONGOZI wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania-Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, iwasilishe ombi lao Mahakama Kuu ya Tanzania la kupinga matamshi yaliyotolewa na Taasisi ya Serikali, dhidi ya mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi yanayowakabili mahakamani hapo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limewasilishwa mahakamani hapo leo Ijumaa, tarehe 13 Agosti 2021 na mawakili upande wa utetezi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba.

Akiwasilisha ombi hilo, Wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala, amedai matamshi hayo ambayo hakuyataja, yataathiri mwenendo wa kesi hiyo.

Amedai, wateja wake wanayaona matamshi hayo kama hukumu, hivyo hawana imani kama mashtaka yao yataendeshwa kwa uhuru mahakamani.


"Tumeleta taarifa ya kusudio la kuiomba mahakama ipeleke Mahakama Kuu kama suala la kikatiba, matamshi yaliyotolewa na taasisi fulani hapa nchini, watu wote wanaifahamu, wamesikia.

"Tunachosema maneno yale au matamshi yale kwa maoni yetu sisi na wateja wetu, yameingilia uhuru wa mahakama. Sio mahakama hii tu, lakini mahakama itakayokwenda kusikiliza shauri la ugaidi linalowakabili washtakwia," amedai Kibatala.

Katika maombi hayo, Mbowe na wenzake, wanaiomba Mahakama Kuu iangalie kama matamshi hayo yameingilia uhuru wa mahakama na kama itabainika yameingilia uhuru wa mhimili huo, kesi husika ifutwe.


"Kwa kuwa mamlaka ile yenye nguvu naishawishi basi matamshi yale kwa namna yalivyotamkwa, yamewafanya wateja wetu kuona tayari wamehukumiwa na kwamba hakuna namna yoyote wanaweza wakapata fair trial, tumeomba iangalie matamshi yale kama yameingilia uhuru wa mahakama," amesema Kibatala.

Kibata ameongeza "na iwapo au la matamshi yale yamesababisha kesi isiwe na mantiki tena na hakuna la kufanya isipokuwa kufutwa."

Kibatala amesema hayo nje ya Mahakama hiyo baada ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 27 Agosti 2021.

Awali, Wakili wa serikali Pius Hilla, alisema kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini washtakiwa wameshinmdwa kufikishwa mahakamani kutokana na kukosekana usafiri jambo lililopingwa na Kibatala, akisema walipaswa kuletwa mahakamani na si kama walivyofanya.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...