MSAJILI wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Vickness Mayao amezindua rasmi Wiki ya AZAKI inayotarajiwa kufanyika Oktoba 25 hadi Oktoba 29 mwaka huu huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wapya wa Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali kupitia Mwenyekiti na timu yake yote.
Akizungumza leo Julai 29,2021 jijini Dar es Salaam wakati akizindua wiki hiyo ya AZAKI,Mayao amesema hiyo ni mara yake ya pili sasa kupata nafasi ya kukutana na wakuregenzi wa Asasi za kiraia nchini pamoja na wadau wengine wa maendeleo, baada ya mkutano wa kikao kazi uliofanyika Januari mwaka huu.
"Ama kwa hakika fursa hizi za kukutana nanyi zimeendelea kuwezesha uimarikaji wa mahusiano na mashirikiano kati ya asasi za kiraia na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini. Nichukue nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa mara nyingine tena kwa uongozi mpya wa Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kupitia Mwenyekiti na timu yake yote.
"Wizara Pamoja na ofisi yangu tulipata faraja kubwa kuona kuwa sasa uongozi na uratibu wa sekta ya asasi za kiraia nchini umerejea mahali pake. Sote ni mashahidi wa madhara yaliyojitokeza kutokana na ukosefu wa uongozi na uratibu wa sekta ya asasi za kiraia nchini kwa miaka kadhaa.Nipende kuwaahidi kuwa ofisini yangu iko tayari kushirikiana nanyi kwa karibu sana kuhakikisha ustawi na usimamizi dhabiti wa sekta ya asasi za kiraia nchini,"amesema.
Aidha ametoa pongezi kwa Kamati ya uchaguzi wa NaCoNGO chini ya Mwenyekiti wake Flaviana Charles wakili msomi na uratibu makini wa mchakato mzima kupitia Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society Francis Kiwanga."Hakika mmedhihirisha bayana nguvu ya umoja na mshikamano ambayo ikiendelea kutumika vizuri itapelekea mapinduzi na maendeleo ya hali ya juu kwa sekta hii ya Asasi za kiraia nchini."
Kuhusu Wiki ya AZAKI , Mayao amefafanua wamekutana kwa ajili ya tukio muhimu kwa wadau wa maendeleo nchini ikiwemo Asasi za kiraia, sekta binafsi, pamoja na Serikali ambayo ndio mdau mkubwa wa maendeleo katika taifa letu. "Sote ni mashahidi wa umuhimu na matokeo chanya ya Wiki ya AZAKI toka uzinduzi wake mwaka wa 2018, ikiwemo kuongezeka kwa umoja na mshikamano miongoni mwa wadau wa maendeleo.
"Kuimarika kwa mshikamano kati ya Asasi za kitaifa na za ngazi ya jamii/mashinani, asasi za wazawa na mashirika ya Kimataifa, wakala wa sekta binafsi pamoja na taasisi za serikali na vyombo vya maamuzi.Tunashuhudia pia kuimarika kwa ushiriki wa Asasi katika masuala ya kisera kwa kujiamini zaidi na kwa kushirikiana na vyombo vya serikali pamoja na Bunge katika misingi ya kuaminiana,"amesema.
Aidha kupitia Wiki ya AZAKI, wameona kuongezeka kwa ushirikishanaji taarifa na upashanaji habari miongoni mwa wadau wa maendeleo. Pia kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa Jamii ya Watanzania kuhusu kazi na huduma zitolewazo na Asasi za kiraia na wadau wa maendeleo, sambamba na mchango wao katika ujenzi wa Taifa.
"Kwa miaka miwili mfululizo 2018 na 2019, Wiki ya AZAKI ilifanyika Jijini Dodoma na kuwaleta kwa pamoja wadau muhimu wa maendeleo. Zaidi ya Asasi 1,000 kutoka mikoa yote nchini zimeshiriki katika jukwaa hili tena kwa kujigharamia ushiriki wao katika warsha na maonesho ya kazi za Asasi za kiraia.Kauli mbiu ya Wiki ya AZAKI kwa mwaka 2018 ilikua "Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Watu, Sera na Utekelezaji". Ambapo kwa mwaka 2019 kauli mbiu ilikua "Ubia kwa Maendeleo: Ushirikiano kama Nguzo ya Maendeleo nchini Tanzania.
Ameongeza kauli mbiu ya mwaka huu ni mchango wa sekta ya Asasi za kiraia katika maendeleo ya nchi, kwa ufupi AZAKI na maendeleo huku akisisitiza Wiki hiyo ya AZAKI inatarajiwa kufanyika mwezi wa Oktoba 25 - 29 Jijini Dodoma, ikitanguliwa na maonesho ya kazi za Asasi za kiraia nchini Oktoba 23 na Oktoba 24 mwaka huu.
Amesema Wiki ya AZAKI ya mwaka 2018 ilileta mwamko mkubwa miongoni mwa wadau wa sekta kuonesha na kuudhihirishia umma wa watanzania mchango wa AZAKI katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Miongoni mwa jitihada zilizochukuliwa ni kutoa ripoti ndogo ya mchango wa AZAKI katika uchumi wa Taifa.
"Niwahakikishie kuwa ofisi yangu, kwa kushirikiana na NaCoNGO pamoja na wadau wa kamati ya maandalizi itahakikisha ripoti hii inakamilika kwa wakati na kuwasilishwa katika wiki ya AZAKI mwezi Oktoba mwaka huu 2021,"amesema.
Aidha amesema toka kuanzishwa kwa Wiki ya AZAKI Ofisi ya Msajili imekuwa ikishiriki kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wa shughuli hii muhimu, kama mshauri mkuu kwa kamati ya maadalizi. "Mwito wangu kwa kamati ya maandalizi ni kuendelea kuboresha ushirikiano wao kuhakikisha AZAKI zinakua imara na zinaleta mchango unaostahili katika maendeleo ya nchi".
Kwa upande wake Mwenyekti wa Bodi wa Baraza la Uratibu wa NGOs Taifa Lilian Badi amesema ni mara yake ya kwanza kukutana na wadau hao tangu yeye na wenzake 29 wachaguliwe kutoka mikoa 26 na wawakilishi wanne wa makundi maalum kuwa wajumbe wa baraza la uratibu wa NGOs Tanzania.
Aidha amesema ni muhimu kutambua kwa miaka mingi sasa Foundation for Civil Society imekuwa kinara katika kuzijengea uwezo NGOs kupitia ruzuku na hata kuwapatia mafunzo mbalimbali na kuwaunganisha kwa njia kadhaa."Na leo hii tunapozindua wiki ya AZAKI ni ushahidi tosha kuhusu ufanisi na dhamira yetu ambayo haijawahi kupwata na tunajua tukio hili mmekuwa mkilifanya kila mwaka."
Ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa Foundation for Civil Society na wadau wengine waendelee kuunga mkono chombo hicho muhimu kilichoundwa kisheria kwa kuhakikisha sio tu kinafanya kazi zake kwa ufanisi bali NGOs zinaelewa majukumu na nafasi ya NaCoNGO kisheria na kiuendaji ili kuepuka chombo hicho kujikuta kwenye migogoro ya mara kwa mara na isiyo na tija au kudhoofika.
Awali Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) anayewakilisha Asasi za kiraia amesema ameshauri vitu vya tatu, cha kwanza wakati umefika fedha za ufadhili ambazo zinakuja kwa ajili ya ASASI za kiraia zitekeleze mipango iliyopo kwani takwimu zinaonesha fedha hizo zinapoingia ni asilimia moja tu ndio inakwenda kwenye NGOS za ndani na iliyobakia inakwenda kwenye mashirika ya kimataifa, hivyo umefika wakati ASASI za kiraia nchini kushiriki kikamilifu kwenye maendeleo.
Amesema eneo la pili ambalo ameshauri ,amesema sekta ya AZAKI mara nyingi inahesabiwa kama sehemu ya sekta binafsi, lakini sekta binafsi ni tofauti ambayo inawafanyabishara zaidi na anapokwenda kuongea mwakilishi wa seta binafsi hawezi kuwa anawakilisha sekta ya AZAKI, hivyo ni vema AZAKI nao wakatambula na mwisho amesema bado kunachangamoto katika kufanya kazi wao kama sekta hasa katika kutekeleza matakwa ya kisheria hasa sheria za kodi.
"Kuna mkanganyiko mkubwa kwa mfano unakuta mimi ni mkurugnzi natumia vijana wanaojitolea lakini unapowalipa posho TRA anahesabu wale kama wafanyakazi kitu ambacho sio sahihi, kwa hiyo bado kuna mkanganyiko wa uelewa wetu katika sheria ya kodi kwa mashirika ambayo sio ya kiserikali na hiyo inachangia sisi kukwama."