Saturday, July 3, 2021

Viongozi wa Afrika waungana na Wazambia kumuaga Kenneth Kaunda


Wanajeshi wakibeba jeneza la Kaunda, LusakaImage caption: Wanajeshi wakibeba jeneza la Kaunda, Lusaka

Viongozi wa Afrika wamejumuika na wananchi wa Zambia katika ibada ya mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hilo, Kenneth Kaunda.

Marais kutoka Ghana, Kenya, na Zimbabwe ni miongoni mwa viongozi wakubwa kutoka Afrika waliohudhuria ibada hiyo ya kumuaga muasisi huyo na mmoja na wapigania uhuru mashuhuri Afrika.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ni miongoni mwa waliohudhuria ambapo mtandao wa Ikulu yake ulichapisha picha za matukio yanayoendelea Lusaka.

Kaunda alipigiwa mizinga 21 ya heshima, huku ndege za kijeshi zikiruka juu ya uwanja huko Lusaka kama sehemu ya heshima kwa mkuu huyo wa zamani wa nchi, aliyefariki dunia akiwa na miaka 97.

Jeshi la Zambia limekuwa likiupitisha mwili wake katika mikoa 10 ya nchi hiyo ili kuwapa nafasi wananchi kutoa salama zao za mwisho.

Katika hotuba yake hapo jana kwa taifa hilo, Rais wa Zambia Edgar Lungu, alisema siku ya leo itakuwa mapumziko ili kutoa nafasi kwa wananchi wengi kzaidi ushiriki kwenye ibada hiyo, kupitia televisheni.

Kaunda atazikwa Julai 7 mwaka huu katika maziko ya faragha yatakayohudhuriwa na watu wachache wa familia na viongozi wa juu.




Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...