Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile, amewasisitiza Watanzania kuendelea kuhakiki namba zao za simu na kutumia mitandao vizuri ili kuepukana na wimbi la uhalifu wa mtandaoni ambao serikali inakabiliana nao kwa sasa.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo katika uzinduzi wa tovuti na mpanago mkakati wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, jijini Dodoma na kueleza kuwa ili kudhibiti utapeli wote kwa njia ya mtandao kwa sasa wanaelimisha umma ili baadaye waanze kuchukua hatua kali.
"Niwaombe Watanzania, kila mmoja ahakiki namba zake za simu, namba ambayo hauitambui nenda kaifute ndio hizo zinatumika na matapeli, na usikubali kubonyeza alama ya kidole zaidi ya mara moja kwa sababu kila unapobonyeza zaidi ya mara moja huo ni usajili tofauti," amesema Dkt. Ndugulile.
"Nitoe rai tutumie mitandao kwa njia sahihi, tunapata shida sana sisi kama serikali, na kuna watu hawana uelewa sheria zipo, wewe unabifu na jirani yako unaenda kwenye ukara wa Instagram unamchamba hilo kosa, usifikiri hata ukitumia fake name hatuwezi kukujua tutakujua tu na tunaweza tukakufikia vilevile" aliongeza Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt. Ndugulile amewakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika 5G huku akibainisha lengo la serikali la kuindokana na intaneti ya 2G ili kiwango cha chini kiwe cha 3G.
"Sasa hivi tunataka tuondokane na 2G tuingie angalau kwa kiwango cha chini cha 3G, serikali imeondoa kodi na sisi kama serikali tunataka mtu yeyote akiwa ndani ya nchi yetu kokote kule alipo aweze kutumia simu janja na aweze kutumia Intaneti," amesema Dkt. Ndugulile.
Mwezi Januari, 2020 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania nchini TCRA ilitoa utaratibu wa uhakiki wa laini za simu ambao unaendelea kutumika hadi leo ukiwa na lengo la mtumiaji kujua ni namba ngapi zimesajiliwa na kitambulisho chake cha NIDA, kwa kufanya hivyo kutahakiisha usalama wake pamoja na kukabilana na wizi wa mtandaoni.