Uamuzi wa wengi wa mahakama ya juu zaidi ya Afrika Kusini kumhukumu Jacob Zuma kwa miezi 15 gerezani ulikuwa "wa mihemko na wenye hasira na usio sawa" na katiba, taasisi ya rais huyo wa zamani imeeleza.
Mahakama ya kikatiba Jumanne ilimkuta na hatia Bw. Zuma kwa kukaidi amri ya mahakama ya kumtaka kufika mahakamani kujibu tuhuma za rushwa wakati alipokuwa rais.
Mahakama imempa siku tano za kujisalimisha polisi.
Katika taarifa iliyotolewa usiku, mfuko wa Jacob Zuma ulisema kuwa mawakili wa Zuma punde watatoa ''ushauri wa kisheria kuhusu mkondo wa kufuata''.
Rais huyo wa zamani alitoa ushahidi wake mara moja tu wakati wa uchunguzi lakini akakataa kujitokeza tena baadaye.
Tume ya uchunguzi iliyoongozwa na jaji Raymond Zondo – aliitaka mahakama ya kikatiba kuingilia kati.
"Msimamizi wetu ameelezea mashaka yake juu ya uhalali wa Tume ya Zondo, upendeleo ambao unaoneshwa, na ukweli kwamba imebadilishwa kuwa 'machinjio' na jukwaa ambalo kila aina ya madai yasiyothibitishwa na ya kukashifu yamefanywa dhidi yake, " taasisi hiyo ilisema.