Burundi imeridhia kupokea chanjo ya Covid , lakini serikali haitawahamasisha watu kupata chanjo hiyo, waziri wa afya nchini humo ameeleza.
Dkt Thaddée Ndikumana amewaambia waandishi wa habari kuwa chanjo hizo zimependekezwa na Benki ya Dunia na wakachukua uamuzi wa ''kuzikaribisha''.
Aliongeza, hatahivyo serikali haitahamasisha watu kuchoma chanjo, bali kila atakayehitaji ataifuata chanjo hiyo.
Mamlaka ya Burundi wamekuwa na wasiwasi kuhusu kupokea chanjo hizo, na hapo awali walisema watafuatilia ufanisi wa chanjo katika maeneo mengine, kabla ya kuzikubali nchini.
Katika mkutano na wanahabari Alhamisi jioni, waziri alithibitisha ripoti kuwa maambukizi ya virusi vya corona yameongezeka katika wilaya za kaskazini zilizo maeneo ya mpakani na Rwanda, na mji wa kibiashara wa Bujumbura.
Kwasababu hiyo, amesema watafungua vituo vya tiba katika mikoa iliyoathirika.
Wizara ya afya ya Burundi hadi sasa imeripoti maambulizi karibu 6,000 vya Covid tangu janga hilo lilipoingia nchini humo mwezi Machi 2020.