Tuesday, June 1, 2021

TMA yatoa tahadhari ya kipupwe na baridi



Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mikoa mitano ya Nyanda za Juu Magharibi kunatarajiwa  kuwa na nyuzi joto kati ya sita na 14 na kusababisha  vipindi vya baridi kali  kuanzia Julai,  2021.

Akitoa  mwelekeo wa utabiri mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema baridi na kipupwe  kinachotarajiwa kuanzia Juni hadi Agosti,  2021 hali ya joto la chini linatarajiwa kuwa ya kawaida na vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kujitokeza kuanzia  Julai, 2021.

DK Kijazi ameitaja mikoa ambayo itatarajiwa kuwa na nyuzi joto sita hadi  14 ni Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Kusini mwa Morogoro.

Amesema hali ya joto la chini linatarajiwa kuwa la juu kidogo ya kiwango cha kawaida katika maeneo ya Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Tanga na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba kati ya nyuzi joto 18 na nyuzi joto 23.

Dk Kijazi amesema Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara inatarajiwa kuwa kati ya nyuzi  joto 10 na 17 huku Mikoa ya Ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Shinyanga na Simiyu ikitarajiwa kuwa na nyuzi joto14 na nyuzi joto 19.

Hali ya joto la chini linatarajiwa kuwa nyuzi joto la kawaida kati 10 na nyuzi joto 17 kama ilivyozoeleka katika maeneo ya Kanda ya Kati kwenye mikoa ya Dodoma na Singida.

"Mkoa wa Ruvuma inatarajiwa kuwa na nyuzi joto 14  hata hivyo vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kuwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini Magharibi hususani nyakati za usiku na asubuhi," amesema Dk Kijazi.

DK Kijazi amesema kutokana na utabiri huo hali mbaya ya joto la chini ya kawaida inayotarajiwa hasa maeneo ya miinuko inaweza kuleta athari kwa binadamu,wanyama, samaki na ustawi wa mazao.

Amesema kwa upande wa hali ya joto Bahari ya Hindi inatarajiwa kuwa juu ya wastani hivyo ongezeko kidogo la joto la bahari linatarajiwa kuongezeka hivyo  samaki wataongezeka.

Pia Dk Kijazi amewataka wananchi kufuatilia utabiri huo wa msimu wa Juni-Agosti  ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha Juni na Agosti,  2021 inatarajiwa katika maeneo mengi nchini kuwa na vipindi vya upepo mkali wa kusi.

"Kwa kawaida msimu wa kipupwe hutawaliwa na upepo wa kusi, kutokana na matarajio ya uimarikaji wa wastani wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa Afrika vipindi vichache vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, " amesema Dk Kijaji.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...