Tuesday, June 29, 2021

TAASISI YA WAJIBU YAZINDUA RIPOTI ZA UWAJIBIKAJI MWAKA 2019/2020, WADAU WAPONGEZA

WADAU mbalimbali kutoka taasisi za Serikali, viongozi, wabunge ,Asasi za Kiraia na wanafunzi vyuo vikuu wameshuhudia uzinduzi wa Ripoti tano za Uwajibikaji ambazo zimetokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali( CAG).

Ripoti hizo zimeandaliwa na Taasisi ya WAJIBU ambayo imeziandaa ripoti hizo za uwajibikaji baada ya kuichambua kwa kina ripoti ya CAG ambayo iliwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 28 mwaka huu na baadae ripoti hiyo ya CAG ikakabidhiwa kwa Bunge Aprili 4 mwaka huu.

Akizungumza jana Juni 28,2021 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya WAJIBU,Bwa. Ludovic Utouh ambaye amewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), amesema ripoti hizo ni za tano tangu waanze kuandaa na kuzitayarisha kutokana na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

"Kama tunavyojua ripoti za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambazo zimewasilishwa kwa Rais Machi 28 na kuwasilishwa bungeni Aprili 4, ni ripoti zinazotayarishwa kitaalamu, ni ripoti kubwa na ripoti ambazo kusema kweli kwa Watanzania wangi huwa hawana shauku ya kuisoma kwa sababu ya ukubwa wake.

"Sasa sisi WAJIBU tunachukua ripoti zile na kuchambua kwa undani na tunachukua yale tunayoamini yanauzito na umuhimu mkubwa kwa watanzania, kwa hiyo utakuta ripoti ya WAJIBU iliyozinduliwa leo ya Serikali kuu na mashirika ya umma inatokana na ripoti mbili kubwa za CAG za Serikali Kuu na mashirika ya umma na tumeweza kuja na kitabu cha kurasa 31.

"Na utakuta katika ripoti ile kubwa tumechambua mambo 10 ambayo tumeona yana umuhimu zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu na ukienda kwenye ripoti ya serikali ya mtaa na miradi ya maendeleo ambayo nayo imetokana na ripoti mbili za CAG ambayo ina mambo 21 ina mambo nane ambayo tumeona yana umuhimu kwa umma.

"Ukija kwenye ripoti ya tatu ambayo ni ripoti ya Ufanisi ile kwa kuwa imetokana na ripoti ya CAG mwaka jana aliwasilisha bungeni ripoti 15 za ufanisi, sisi katika kupitia ripoti zile tumeona zina mambo muhimu zaidi kwa maendeleo ya nchi na tumeweza kuja na ripoti yenye page 31 ambayo inajikita kwenye maeneo hayo, "amesema Utouh.

Amesema ombi lake baada ya kuzinduliwa kwa ripoti hizo za uwajibikaji, ni vema wananchi wakazisoma kwani watazisambaza katika maeneo mbalimbali na zitakuwepo kwenye Website ya WAJIBU ,pia zitapatikana kwenye taasisi.

"Tutazigawa kupitia taasisi mbalimbali ili watanzania wapate ripoti hizi na wazisome, wakati tunasherehekea siku 100 za uongozi wa Rais Samia kweli sisi kama wananchi wa Tanzania tuwe na ari ya kuungana naye na kumsaidia kwa nia yake njema aliyonayo ya kuleta maendeleo ya nchi katika kudai uwajibikaji pale.

"Ambapo tunaona taasisi ya serikali au chombo cha Serikali hakitimizi wajibu wake , ndio lengo la WAJIBU tunasema kwamba rasimali za Serikali za taifa zikisimamiwa vizuri zinakuwa za kila Mtanzania.

Kwa upande wake Mwakilishi Ofisi ya Msajili wa NGO's Charles Mpaka amewapongeza WAJIBU kwa kuja na ubunifu waliokuja nao wa kupitia ripoti ya CAG na kuziandikia taarifa fupi ."Tumeona ripoti ya CAG ni kubwa na WAJIBU wameona umuhimu wa kuichambua na kuja na taarifa fupi.Ripoti ya CAG ilikuwa na zaidi ya kurasa 250 lakini wao wamekuja na taarifa yenye 21 mpaka 31.

"Maana yake tunaongea asilimia nane mpaka 11 wamekwenda kuipunguza, hivyo itakwenda kusaidia wananchi kupata tafsiri ya haraka na uelewa mwepesi wa ripoti ya CAG,"amesema

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe.​Naghenjwa Kaboyoka amesema wamekuwa wakifanya kazi na WAJIBU kwa karibu sana na kwamba WAJIBU wamekuwa kama Bunge nje ya Bunge, wamekuwa wakiwakilisha wananchi , maana hizo ripoti zao wanazichambua kiasi kwamba wananchi wanaweza kuzisoma na kuzielewa.

"Kwa hiyo imekuwa mkono wetu wa kulia wa kusaidia kamati zetu mbili za PAC na LAAC , unakuta wenzetu wanakwenda mbali zaidi kueleza yale ambayo hatupati muda wa kuyazungumzia bungeni lakini wenzetu WAJIBU wanayachambua na kuyaeleza kwa wadau, na hivyo wadau wanapata nafasi ya kujua kilichopo.

"Kwa mfano tukiangalia bajeti ya mwaka huu siku zote tunasema kilimo ndio uti wa mgongo lakini akangalia bajeti iliyopita nafikiri ilitolewa tu asilimia mbili na hii ndio sekta ya uzalishaji, sasa kama sekta ya uzalishaji hazitatengewa hela nyingi zikazalisha tunategemea maendeleo gani, yatakuwa maendeleo ya vitu sio watu.

"Serikali za mitaa tuna tatizo moja, tatizo linawezekana hawa wanzetu tangu wamemaliza shule hajawahi kupelekwa kozi , hajui tena taratibu za kimataifa za kutoa ripoti zimekuaje , matokeo yake inawezekana kweli hajaiba lakini akawa hajui jinsi ya kuandaa ripoti, kwa hiyo anapata ripoti chafu.

"Lakini kusema kweli ni vizuri hawa wenzetu ambao wapo katika taaluma ya kusimamia masuala ya fedha mara kwa mara wapelekwe kwenye kozi, mara kwa mara waelezwe taratibu mpya na kufundishwa ,maana unakuta wanasema hawa wamezoea kuandika vocha tu,"amesema.

Ameongeza inawekana ni wasomi wazuri lakini viwango vya kimataifa vya kuandaa ripoti ambavyo vimewekwa havijui , hivyo halmashauri inapata hati chafu, mwingine anapata hati safi na anayepata hati safi haina maana mambo yao ni mazuri kuliko aliyepata hati chafu."Lakini ina maana gani , hesabu zao hawajazifunga kwa utaratibu unaokubalika kimataifa".

Aidha amesema anashukuru kusikia kuna halmashauri ambazo zimeanza kuchukua hatua za kuwapeleka watu wao wa kuandaa ripoti kupata kozi za kuwaongezea ujuzi huku akieleza CAG anaweza kusaidia hao watu wakaelekezwa namna ya kufunga hesabu.
Mwakilishi Ofisi ya Msajili wa NGO's Charles Mpaka (kushoto) akikata utepe kwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya WAJIBU,Bwa. Ludovic Utouh (kulia) kuashiria uzinduzi wa ripoti za Uwajibikaji mwaka 2019-2020 jijini Dodoma,huku tukio hilo likishuhudiwa na Wadau wengine mbalimbali zikiwemo taasisi za Serikali, viongozi, Wabunge,Asasi za Kiraia na wanafunzi vyuo vikuu.
Mwakilishi Ofisi ya Msajili wa NGO's Charles Mpaka (kushoto) kwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya WAJIBU,Bwa. Ludovic Utouh (kulia) wakiangalia vitabu vya ripoti hizo namna ya kuwagawia Wadau mbalimbali walioshiriki kwenye uzinduzi wa ripoti za Uwajibikaji mwaka 2019-2020 jijini Dodoma.

WADAU mbalimbali kutoka taasisi za Serikali, Wabunge ,Asasi za Kiraia na wanafunzi vyuo vikuu ambao wameshuhudia uzinduzi wa Ripoti hizo,wakipitia kwamakini Ripoti hiyo mara baada ya kuzinduliwa rasmi jijini Dodoma.
Picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya WAJIBU,Bwa. Ludovic Utouh akizungumza jambo mbele ya Wadau mara baada ya ripoti hiyo kuzinduliwa
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...