Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza msururu wa masharti mapya ya kupambana na ongezeko la visa vya virusi vya Corona nchini humo. Hatua hizo zilianza kutekelezwa saa kumi jioni (EAT) jana tarehe tarehe 18 Juni.
Kwenye hotuba iliyopeperushwa kupitia runinga Ijumaa usiku, Museveni alitangaza kuwa usafiri wote wa kibinafsi na wa umma nchini umepigwa marufuku kwa siku 42 zijazo isipokuwa kwa huduma muhimu na mizigo.
Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Entebbe na vivuko vingine vya mpaka wa ardhi hata hivyo vitabaki wazi kwa watalii na wale wanaorejea lakini mamlaka zimepewa jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna kesi chanya au aina mpya za covid zinazoingia nchini humo .
Amri ya kutotoka nje imesongeshwa kutoka saa tatu usiku hadi saa moja usiku na itadumu hadi saa kumi na moja unusu alfajiri .Waendeshaji pikipiki, wanaojulikana kama Boda Boda wanaruhusiwa kubeba bidhaa tu.
Kazi zote zinazozingatiwa sio za lazima, shule na taasisi za kujifunzia, sehemu za ibada, na hafla za michezo pia zimefungwa kwa siku 42 zijazo.
Vituo vya biashara na maeneo ya biashara pia yamefungwa na wachuuzi wa soko wakiruhusiwa kulala kwenye vibanda vyao.
Uwanja wa ndege wa kiamaifa wa Entebbe na maeneo ya biashara vimefungwa
Museveni alisema hatua hizo ni muhimu kukomesha maambukizi ya sasa ya kijamii na kupeuka kuulemea kabisa mfumo wa utoaji wa huduma za afya.
Katika siku kumi na mbili zilizopita tu, nchi hiyo ilirekodi visa 15 800 na vifo 190 vinavotokana ana Corona .
Rais alionya kuwa kwa kiwango cha sasa cha maambukizo, mahitaji ya oksijeni katika vituo vya afya yangeongezeka mara 9 na nchi haiwezi kukabiliana na hali kama hiyo .
Rais pia ameamuru kwamba wahudumu wa baa na vilabu vya usiku ambao wanapatikana wakipuuza sheria za kufungwa wapokonywe leseni za kuhudumu
Baa na sehemu za burudani zilifungwa rasmi Machi 2020, lakini zingine zimekuwa zikifanya kazi kinyume cha sheria. Wale watakaopatikana wakihudumia wateja sasa watakamatwa na kutakiwa kulipa faini kubwa.
Idara za serikali zitakuwa na asilimia 10 tu ya wafanyikazi wao wanaofanya kazi kutoka ofisini.
Tangu mwishoni mwa Mei wakati nchi iliingia wimbi lake la pili,visa vya Corona vimekuwa vikiongezeka haraka. Katika mji mkuu Kampala, zaidi ya visa 15,300 vimerikodiwa katika siku ishirini na moja zilizopita na jumla ya visa 9000 hurekodiwa kila wiki nchi nzima.
