Monday, June 28, 2021

Dc Busega aanza na kwa kusimamia ushuru wa ndani


Mkuu wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu Gabriel Zakaria  amesema atahakikisha anasimamia  makusanyo (ushuru) ndani ya Wilaya hiyo ikiwa ni moja kati ya vipaumbele vyake atakavyovitekeleza akiwa Wilayani hapo.

 Mkuu huyo alisema hayo jana wakati wa kikao chake na wananchi wa kijiji cha Bukabile kata ya Nyashimo ,kilichofanyika katika viwanja vya standi Wilayani hapo.

Alisema bila kusimamia makusanyo ya ushuru,wilaya hiyo haiwezi kuwa na miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo ataanza na usimamizi madhubuti wa ushuru kwa kuunda kikosi kazi cha ufuatiliaji na ukusanyaji.

"Suala la ushuru( mapato) kwangu mimi ni kipaumbele cha kwanza na nitahakikisha tunakusanya zaidi ili asilimia 40 ya miradi iweze kubaki kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za jamii" alisema.

Aliongeza kuwa Wilaya ya Busega ina vyanzo vingi vya makusanyo na kwa kutumia vyanzo  hivyo wataweza kukusanya fedha zaidi na wananchi watapata huduma za afya,miundombinu na elimu .

Aidha amewataka wananchi kulipa kodi wanazostahili na kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kwa pamoja waweze kuibadilisha wilaya hiyo na kwa Wilaya ya mfano.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...