Sunday, May 30, 2021

Wakulima ufuta watakiwa kulinda ubora

 


Mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amewataka wakulima wa ufuta,  washiriki kikamilifu kulinda na kudhibiti ubora wa ufuta ili kupata soko la uhakika.


  Ndemanga ametoa wito huo akiwa   katika kijiji cha Kilangala B, jimbo la Mchinga.


Amesema ili kulinda na kupata soko zuri,  ni vyema wakulima wakazingatia  usafi wa mazao yao. Pia  aliwataka wanunuzi wazingatie na kutekeleza kwa vitendo makubaliano,  ikiwamo kuwalipa wakulima kwa wakati kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kuhusu muda wa malipo baada ya kushinda mnada.


Ndemanga pia amekitaka chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao kuhakikisha kina vifungashio vya kutosha ili ununuzi usisimame.


Mnada huo wa kwanza ni kwa chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao, ambao ni muunganiko wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) vilivyo katika wilaya za Lindi na Kilwa.


kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Chama kikuu Lindi Mwambao Ismail Nalinga, amesema  chama hakitawavumilia viongozi na watendaji watakaochafua soko kwa kuchanganya mchanga na ufuta.


''Ipo tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji ya kuongeza mchanga kwenye ufuta,  hatutawavumilia na tutawachukulia  hatua za kinidhamu,'' amesema Nalinga.


Mnada wa mauzo  wa ufuta umeanza, huku  tani 1370 zikiuzwa kwa bei ya chini ya Sh2,201  na juu Sh2,345.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...