Saturday, May 29, 2021

Serikali kuandaa Sera itakayowawezesha Vijana kiuchumi

 


Na John Walter-Manyara

Katika kuhakikisha lengo la kukuza uchumi wa viwanda linatimia, Serikali ya Tanzania inaendelea kubuni sera na mikakati ya kukuza uwekezaji kupitia wajasiriamali wadogo.


Hayo yamesemwa na Naibu waziri wa Viwanda na biashara Exaud Kigahe wakati akifungua maonesho ya 16 ya SIDO kanda ya kaskazini yanayofanyika katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara.


Amesema serikali inaandaa sera mpya  ya maendeleo ya Viwanda vidogo na biashara ndogo ambayo pamoja na mambo mengine imetazama namna bora ya kuwawezesha wajasiriamali vijana kuingia katika shughuli za kiuchumi.


Aidha amesema serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kuwawezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa katika kukuza fursa za masoko kwa kuendelea kupanua wigo mpana wa masoko katika jumuiya ya Afrika Mashariki,nchi za SADC, ambapo pia kwa sasa serikali ipo katika hatua za mwisho kulipia mkataba wa eneo huru la biashara Afrika.


Amewataka wajasiriamali kutumia masoko hayo kikamilifu ili serikali ipate nguvu ya kuendelea kuwatafutia fursa zaidi.


Kagahe amesema sekta ya Viwanda na Biashara nchini imeendelea kuongeza miundombinu ya kufanyia kazi wajasiriamali wadogo katika mitaa ya viwanda vidogo vya SIDO ambapo mpaka sasa imejenga zaidi ya majengo 15 kwenye mikoa ya Manyara, Geita,Kigoma,Mtwara na Dodoma kwa ajili ya uzalishaji, kazi hiyo ni endelevu.


Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya TEMDO iliyo chini ya wizara ya Viwanda na Biashara inayohusika na utafiti,Usanifu na utengenezaji wa Teknolojia mbalimbali Mhandisi Profesa Fredrick Kahimba, amewataka wenye changamoto ya teknolojia kuwasiliana nao ili kupata msaada na biashara zao kupata tija.


Amesema katika kuwafikia wajasiriamali wadogo wanawatembelea katika mikoa mbalimbali na kupitia mtandao wa  SIDO.


Maonesho hayo ya 16 ya SIDO  yanabebwa na kauli mbiu isemayo Maendeleo ya viwanda nuru ya maendeleo kiuchumi,yanatarajiwa kufungwa mei 31,2021 na mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...