Wadau wa mafuta ya kula Nyanda za Juu Kusini wakifuatilia kwa karibu mafunzo yaliyotolewa na TBS kwa kushirikiana na BRELA, SIDO na Wakala wa Vipimo.
Wazalishaji wa mafuta ya kula wametakiwa kufuata kanuni bora za kilimo, usindikaji na zile za afya ili kuongeza uzalishaji nanubora wa bidhaa hiyo nchini.
Wito huo ulitolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati wa mafunzo kwa wasindikaji, wauzaji, wasambazaji na wenye maduka yanayouza mafuta wapatao 972 yaliyofanyika katika mikoa minne ya nyanda za juu kusini kuanzia February 19 hadi 29 mwaka huu.
Mafunzo hayo yalihusisha wadau hao kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutaka wazalishaji wa mafuta nchini kusaidiwa ili waweze kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyi.
Kwa sasa mafuta ya kula yanayozalishwa nchini ni tani 200, 000 kwa mwaka, wakati mahitaji halisi ni kati ya 400,000 hadi 600,000.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na BRELA, SIDO na Wakala wa Vipimo (WMA), ambapo kila mmoja alieleza wadau hao nafasi yake katika kufanikisha uzalishaji na ukuzaji biashara ya mafuta.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Udhibiti Ubora wa Bidhaa TBS, Baraka Mbajije, aliwataka wazalishaji wa mafuta kufuata kanuni bora za kilimo, usindikaji pamoja na za afya.
Mbajije alisema kanuni bora za kilimo zinahusiha mbegu bora, kuvuna kwa wakati na mazao yanayovunwa kwa ajili ya uzalishaji mafuta yanatakiwa yawe yamekomaa.
Kwa upande wa kanuni bora za usindikaji kwa mujibu wa Mbajije ni pamoja na kuzingatia usafi hasa kwenye mazingira ya viwandani.Alisema mazingira ya uzalishaji viwandani yanatakiwa kuwa safi pamoja na mashine zinazotumika.
Akizungumzia kanuni bora za afya, Mbajije alisema wazalishaji wanatakiwa kuhakikisha vifaa vya kuhifadhi mafuta ni safi ikiwa ni pamoja na madumu yanayotumika kuhifashi mafuta hayo yawe yamesafishwa vizuri.
" Madumu wanayoweka mafuta wahakikishe wameyasafisha vizuri na waweke lebo zinazoeleza bidhaa hizo ni za aina gani," alisema na kuongeza kwamba haikubaliki kwenye vifungashio ambavyo wazalishaji wanaweka mafuta iwe lebo inayohusu bidhaa nyingine.
Aidha, alisema mafuta ya kula hayatakiwi kuwekwa juani, kwani yanapokuwa juani kuna kemikali zinazozalishwa na zinaweza kusababisha magonjwa ikiweno kansa.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Abel Mwakasonda, alitoa mwito kwa wadau hao kusajili TBS majengi ya bidhaa za vyakula na vipodozi.
Alisema kwa kufanya hivyo Shirika hilo litaweza kuwafikia kwa urahisi.
" Tunatoa mwito kwa wadau kufika TBS, wasiogope kama kuna makosa tutawasaidia kuyarekebisha," alisema Mwakasonda.
Alisema ni muhimu kwa wafanyabishara kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na mabadiliko ya Sheria ya fedha ya mwaka 2019.
Sheria hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokua Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA).
Alisema usajili wa bidhaa majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha kufanya biashara zao urahisi.
Usajili majengi ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda kuhifadhiwa humo.
Kwa upande wa usajili wa bidhaa, eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi.Usajili wa vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.
Mafunzo hayo kwa wazalishaji wa mafuta ni mwendelezo wa mafunzo yaliyokwisha kutolewa katika mikoa Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma.
Source