Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Magufuli, leo Ijumaa, Machi 26, 2021, umepumzishwa katika nyumba yake ya milele kwenye makaburi ya familia yaliyopo Chato mkoani Geita.
Majira ya saa 10:50 jioni jeneza lenye mwili wa Hayati John Magufuli lilishushwa katika nyumba yake ya milele na kufuatiwa na tukio la ndugu, viongozi, jamaa na marafiki kuweka mchanga.
Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo akiwa na umri wa miaka 61.
Shughuli ya mazishi hayo imeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mke wa marehemu Mama Janeth Magufuli, marais wastaafu Dkt. Jakaya Kikwete, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.
Mbali na hao shughuli hiyo pia imeshuhudiwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanafamilia, Mawaziri, Makatibu Wakuu, wasanii pamoja na baadhi ya wakazi wa Chato na maeneo jirani.
Shughuli ya maziko iliyofanyika Kijiji cha Mlimani wilayani Chato Mkoa wa Geita katika makaburi ya familia ilihusisha watu wachache wakiwemo viongozi wa Serikali, wastaafu na familia yake.
Majonzi, simanzi na huzuni vilitawala makaburini hapo wakati mwili wa kiongozi huyo ukishushwa kaburini.