NA ANDREW CHALE, CHALINZE
JIMBO la Chalinze linatarajiwa kujengwa jengo la kituo cha huduma za Matibabu ya Dharura 'Emergency Department' litakalosaidia Watanzania mbalimbali ikiwemo wa wanaotoka Mikoa jirani ikiwemo ya Tanga, Morogoro, Dar es Salaam pamoja na Pwani kupatiwa huduma za haraka na za kibingwa pindi wapatapo shida za ajali ama majanga.
Hayo ameyasema Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa kukagua eneo litakalojengwa jengo hilo la mradi huo kwa udhamini wa Shirika la About Fund Tanzania,
ujenzi unaotarajiwa kujengwa eneo la viunga vya Hospitali ya Msoga, Halmshauri ya Chalinze.
"Niwashukuru sana Abbott Fund Tanzania kwa jambo kubwa ambalo wamekuja kutufanyia hapa.
Imekuwa ni kilio cha muda mrefu, kama mnavyofahamu watanzania wengi hasa wanaotoka njia hii ya Tanga, lakini pia wanaotoka njia ya Morogoro kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakipata tabu sana hasa wanapopata matatizo ya kiafya au hata ajali kwa mfano watu wa Tanga wanapopita Kabuku na watu wa upande wa Morogoro wanapoondoka Morogoro, wanapopata shida ya kiafya, Hospitali za karibu zimekuwa mbali sana kwao.
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ilielekeza Halmashauri ya Chalinze, pamoja na kujiandaa kupokea Wilaya lakini ijiandae kuwa sehemu ya 'center' itakayotoa huduma hizo,
hivyo Serikali ilianza kwa kutupatia pesa, kama mnakumbuka zamani hapa kulikuwa na kituo cha afya, lakini serikali ikatoa pesa kukiongeza hadhi kituo hiki kiwe Hospitali.
Majengo mengi yamejengwa, lakini katika jengo ambalo ni muhimu sana ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu ni lile la Huduma za Dharura 'Emergency Department' ambalo sasa leo tumekuja kuangalia na tumekutana na Wakandarasi na Mshauri ambao wamekuja kusimamia ujenzi huo.
Abbott Fund Tanzania wametuhakikishia kwamba watakuwa tayari kutoa pesa za ujenzi wa majengo hayo, pamoja na kuweka vifaa na mahitaji mengine ikiwemo huduma za maji zitakuwepo pale.
Pamoja na jengo lakini wataweka tanki la kuhifadhi maji lita Laki moja, lakini pia wataweka magari ya Wagonjwa 'Ambulance' ambayo yatakuwa yakifika sehemu itakayotokea ajali na kufika kutoa msaada wa haraka". Alisema Ridhiwani Kikwete.
Aidha, Ridhiwani Kikwete aliongeza kuwa;
"Kwangu mimi nisimame kwanza kuishukuru sana Serikali yetu chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutusaidia kutupa mwanga ule wa nini ambacho kipo katika hili, kwa sababu kwa muda mrefu watu wa Chalinze walikuwa wanahitaji huduma hii lakini leo katika awamu ya tano tunakuja kuipata,
Lakini pili kuishukuru pia Abbott Fund Tanzania kwa msaada huu wanaokuja kutupa.... Siku zote usione vyaelea, vimeundwa, waundaji wenyewe wapo, ili jambo nimshukuru sana Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, ambaye yeye ndiye alitufungulia milango ya kuonana nao Abbott Fund na kutupa fursa ya kukutana na leo wamefika kufanya jambo hili". Alisema Ridhiwani Kikwete.
Mbunge pia alitumia fursa ya kuwaasa Wananchi wa Chalinze, kwamba serikali yao inafanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma ya afya lakini kwao wao ni kuona vifaa ama huduma hizo wanazienzi na kuzitunza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmshauri ya Chalinze, Ramadhani Possi, alishukuru Serikali pamoja na Wadau hao, Abbott Fund Tanzania kwa kuweza kutenga fedha za ujenzi wa jengo hilo la dharura katika Halmashauri hiyo.
"Kwa niaba ya Halmashauri ya Chalinze, tunawashukuru sana wadau wetu, Abbott Fund Tanzania, kwa kuja kutujengea jengo hili la dharura hapa kwetu Chalinze.
Hii itatoa suluhisho la matatizo ambalo tulikuwa tunakabiriana nayo kwa upande wa huduma za dharura. Kwa hii ndio itakuwa Halmashauri ya kwanza ya Wilaya kuwa na jengo hili la huduma za Dharura.
Wadau hawa tayari wameshajenga majengo kama hayo ya dharura kwenye mikoa ya Mbeya, Dodoma, Arusha, Tanga na sasa wanakuja hapa kwetu ambapo wametuhakikishia mpaka mwezi Disemba mwaka huu litakuwa limekamilika". alisema Mkurugenzi huyo Ramadhani Possi.
Nae Msanifu wa majengo hayo ya Dharura kutoka Abbott Fund, Bwana. Vasco Bokera alisema ujenzi huo utaanza mara moja ambapo utachukua kuanzia miezi Saba hadi 12 hadi kukamilika kwake kulingana na hali ya hewa na mazingira.