Katibu wa baraza kuu la usalama wa kitaifa nchini Iran Ali Shamkhani amesema leo kuwa mashambulizi ya angani yaliofanywa Ijumaa na Marekani dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika eneo la Mashariki mwa Syria yanachochea ugaidi.
Marekani imesema kuwa mashambulizi hayo katika ngome za wanamgambo hao wa Kataib Hezbollah katika mpaka na Iraq ni kujibu mashambulizi ya roketi dhidi ya malengo ya Marekani nchini Iraq.
Shamkhani amemwambia waziri wa mambo ya nje wa Iraq aliyeko ziarani nchini humo Fuad Hussein kwamba vitendo hivyo Marekani vinaimarisha na kupanua vitendo vya kigaidi vya kundi la itikadi kali la Daesh katika eneo hilo.
Mashambulio hayo ya anga yalilenga maeneo ya wanamgambo katika upande wa Syria katika mpaka kati ya Iraqi na Syria ambapo makundi yanayoungwa mkono na Iran yanadhibiti njia muhimu ya kuvukishwa kwa silaha, wafanyakazi na bidhaa.