Tuesday, January 26, 2021

Waziri Mwambe aonya watakaopandisha bei ya mafuta ya kula kwa sasa


Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Geofrey Mwambe amewaonya wafanyabiashara wa mafuta watakao pandisha bei ya bidhaa hiyo kinyume na bei elekeze kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao za biashara.

Waziri Mwambe ametoa onyo hilo leo  jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari juu ya mfumuko wa bei ya mafuta ambao umekua mkubwa kwa siku za  hivi karibuni.

Amesema kuna uhaba  wa mafuta  nchini na kubainisha kuwa changamoto hiyo itakoma baada ya kuwasili kwa meli mbili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ambazo zimeshusha mafuta takribani Tani 48,000 na uhitaji ukiwa ni mafuta Tank 30,000 kwa mwezi.

"Kwa sasa changamoto ya bei haitakuwepo na tayari tumeshawapunguzia waagizaji baadhi ya gharama za kushusha mafuta pale bandarini lakini pia niwahakikishie watanzania uhaba wa mafuta hauwezi kuendelea kwani Februari 17 kuna meli ya mafuta itawasili na nimeagiza isichukue muda mrefu kushusha pale bandarini hadi Februari 20 meli hiyo iwe imeshashusha mafuta" amesema.

Amewataka watanzania hususa ni vijana kuchukulia changamoto hiyo kuwa fulsa kutokana na kuwa na ardhi inayokubali mazao ya mafuta amesema ni wajibu kwa wakulima kulima kwa wingi mazao hayo.

"Nchi yetu ina ardhi ambayo inakubali kilimo cha mazao ya mafuta, wajiunge kwenye vikundi vidogo vidogo wapatiwe mikopo ile ya kwenye Halmashauri na wajikite kwenye kilimo hiko," amesema Waziri Mwambe.

Aidha waziri Mwambe ametoa maelekezo kwa Tume ya Ushindani kuhakikisha wanafuafitilia mwenendo wa mafuta nchini huku akiwataka kumuandalia ripoti ya hali ya bidhaa hiyo hapa nchini nchini.

Amewataka Wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao ina ardhi inayokubali mazao ya mafuta kama michikichi, alizeti na karanga na mazao mengine ya mafuta kuhamasisha Wananchi wao kujikita kwenye kilimo hicho ili kuweza kujikwamua kiuchumi wao wenyewe lakini pia kuzalisha mbegu ambazo zitatumika na viwanda vya ndani na kupunguza  uagizwaji wa mafuta nje ya Nchi.


Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...