Tuesday, January 12, 2021

TFS Kanda ya Kusini yazindua kampeni ya upandaji miti katika kijiji cha Mijelejele




Na Hamisi Nasri, Masasi 

  WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini imezindua kampeni ya upandaji miti zaidi ya 6000 katika kijiji cha Mijelejele wilayani Masasi mkoani Mkoani Mtwara lengo likiwa ni uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji. 

  Uzinduzi huo ulifanyika jana wilayani Masasi katika kijiji cha Mijelejele kilichopo wilayani humo mkoani hapa, ambapo maafisa wa TFS pia walitumia fursa hiyo kutoa elimu sahihi kwa kufuata kanuni za namna ya upandaji miti kwa mamia ya wananchi wa kijiji hicho waliojitokeza katika uzinduzi huo.

  Akiongea katika uzinduzi huo,afisa misitu na uhifadhi mazingira wilaya ya Masasi,Kelvin Lilai kwa niaba ya afisa misitu kanda ya kusini, Lilai alisema kuwa ili kuweza kuhifadhi na kutunza mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao yaliyowazunguka.

   Lilai alisema TFS imepeleka miti zaidi ya 6000 katika kijiji hicho baada ya kuona kuna uhitaji mkubwa wa upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo ya Mijelejele ikiwemo kwenye vyanzo vya maji,ofisi za umma kama vile Zahanai,ofisi za serikali za vijiji na kwenye barabara za vijiji.

   Alisema katika idadi hiyo ya miti 6000 ambayo wananchi wa kijiji hicho wanatakiwa kuanza kuipanda miti hiyo ni ya aina mbalimbali ikiwemo miti ya kivuli, matunda na mbao ambapo kama ikipandwa na kutunzwa vizuri italeta manafaa makubwa baada ya miaka kadhaa.

   Lilai alisema kwa miti ya kivuli itasaidia utunzaji wa mazingira katika maeneo wanayoishi wananchi na kwa miti ya matunda wananchi watafaidika kupata matunda bora kwa ajili ya kuboresha afya zao na kwa ile ya mbao itawasaidia kupata kipato mara watakavyoanza kuvuna mbao.

  "Lengo la kuleta miti hii 6000 na upandaji miti kwa ujumla ni kutunza mazingira lakini pia kwa matumizi ya baadae kwa ajili ya kujipatia fedha na hata kutunza vile vyetu vya maji katika kuleta uoto wa asili katika nchi yetu hivyo TFS tunatoa wito kwa jamii kuitunza miti ili kuweka mazingira safi,"alisema Lilai

   Alisema lengo la TFS kwa mwaka huu 2021 ni kupanda miti zaidi ya 100,000 katika vijiji vyote vya wilaya ya Masasi na tayari miche zaidi ya 45,000 imeshaoteshwa na kuanza kusambazwa katika baadhi ya vijiji mbalimbali wilayani humo kwa sehemu kubwa kampeni hizo zimekuwa na mafanikio makubwa ambapo idadi kubwa ya miti imeota vizuri.

   Maimuna Husseni mkazi wa kijiji cha Mijelejele alisema kwanza wanaipongeza TFS kwa kuwapelekea miti hiyo kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa wakihitaji ili kuweza kupanda katika mazingira yao kwa lengo la kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji ikiwemo kupata kivuli.

  Lilai alisema mwaka 2019/2020 TFS iliendesha programu ya uhamasishaji upandaji miti kwa upande wa wilaya ya Masasi na jumla ya miche zaidi ya 82,000 ilipandwa katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Masasi

  Akiongea kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho cha Mijelejele,Maimuna Husseni alisema kuwa kwanza wanaipongeza TFS kwa kuwapeleka miche hiyo ya miti kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa wakihitaji ili kuweza kupanda kwenye mazingira yao kwa lengo kuhifadhi mazingira ikiwemo kwenye vyanzo vya maji pamoja na uhitaji wa kivuli.

  Naye diwani wa kata hiyo,Juma Pole aliwataka wananchi wa kata hiyo kuitunza miti hiyo badala ya kuitekeleza kwa sababu kama kila mmoja akiwa makini katika kuitunza miti hiyo yote iliyopandwa katika vijiji hivyo vya kata hiyo hali ya mazingira kwenye kata itakuwa mzuri kimuonekano.

                                  

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...