Na John Walter-Manyara
Migogoro ya ardhi na mirathi katika familia zimetajwa kuwa ni kero na kikwazo katika kuleta maendeleo jambo linalopelekea umaskini katika familia nyingi.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti wakati akisikiliza malalamiko ya wananchi ikiwa ni agizo la Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa Wakuu wa mikoa na wilaya watenge siku ya kusikiliza kero ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.
"Ni utaratibu tuliojiwekea katika mkoa wetu kwamba kila alhamisi ya kila mwisho wa mwezi ndani ya mwaka mzima tusikilize kero za wananchi" alisema Mkirikiti.
Mkirikiti amesema katika malalamiko hayo mengi yalihusu migogoro ya ardhi inayohusu familia ikihusisha ndugu kwa ndugu kushindwa kushirikiana na kufuata utaratibu pindi wanapohitaji kuuza eneo.
Amesema malalamiko mengine yalihusiana na Mirathi ambapo ameelekeza kufuata maelekezo ya mahakama ili kuweza kuepuka migogoro ya aina hiyo.
Pamoja na hayo mkuu wa mkoa alimwagiza mkuu wa wilaya ya Babati Chelestino Mofuga kuhakikisha mzee wa miaka 75 alieleta malalamiko anapatiwa mahali pa kuishi.
Kwa upande wake Mpima ardhi mkoa wa Manyara Stanford Nzowa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la ardhi mkoa wa Manyara amesema migogoro mingine inapaswa kutatuliwa katika ngazi ya Familia kabla ya kufikishwa katika ngazi zingine.
Aidha katika malalamiko hayo waliojitokeza ni pamoja na mwalimu wa shule ya msingi kutoka wilayani Mbulu Peter Kirway ambaye alisimamishwa kazi kwa utoro wa siku 364 na robo akidai kupata hatima yake baada ya kusimamishwa kazi ambapo Mkirikiti ameelekeza mamlaka husika kusimamia miongozo iliyopo.
Akitoa maelezo kwa njia ya Simu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbulu Anna Mbogo amemwambia mkuu wa mkoa kwamba wamemwandikia Mwalimu huyo barua ya kumsimamisha kazi kwa sababu ya Utoro uliokithiri akidai sababu alizotoa mwalimu huyo ni nyumba yake anayoishi mlango hauna komeo.
Naye mwalimu huyo alihoji kuwa adhabu aliyopewa haina kikomo kwa kuwa hatakiwi kutoka nje ya shule bila ruksa maalum.