Msemaji mkuu wa serikali nchini Tanzania Dkt. Hassan Abbas amesema Tanzania inazingatia miongozo yote ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na hata wakati huu ambao dunia inapambana na wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo.
Akihojiwa na kitoa cha redio cha EFM kilichopo jijini Dar es salam, Dkt. Abbas amesema "Sisi Tanzania msimamo wetu ni ule ule,tunafahamu tatizo lipo duniani na dunia inahangaika lakini cha kwanza watanzania waondoe hofu wizara ya afya ilishatoa miongozo, ile miongozo bado ipo haijawahi kufutwa kuna tahadhari za kuchukua hivi wewe kunawa mikono mpaka covid? Alihoji Dkt Abbas.
'' Tulikuwa tuna nawa sana shule baadaye tukaacha kwahiyo kuna zile tahadhari kama alivyosema juzi Mh Rais tuendelee kuzichukua lakini Tanzania tunaamini tumedhibiti haya maambukizi kwa njia zetu za kisayansi na kumshukuru Mwenyezi Mungu''.
''Unajua Tanzania watu wanasahau wanafikiri tulidharau sana huu ugonjwa tulichukua hatua zote dunia ilizokuwa inataka isipokuwa kujifungia ndani maana kuna watu wanatamani sana kufungiwa ndani sijui kuna nini huko ndani" Alisema Bw. Abbas.
Kauli hii inakuja siku moja baada ya shirika la Afya duniani WHO kupitia ofisi yao ya kanda ya Afrika kutoa taarifa ikizitaka mamlaka nchini kujiandaa kupokea chanjo ya corona kama mataifa mengine yanavyofanya na kuikumbusha Tanzania hayo ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa.
Rais Magufuli ameweka wazi chanjo hazifai na kuwataka watanzania kusimama imara na kuwa waangalifu na mambo ya kuletewa huku akiendelea kusisitiza msimamo wake wakutojifungia ndani na kutaka watu kuchukua tahadhari ikiwemo kujifukiza na kumuomba Mungu.
Mapema mwanzoni mwa juma Kanisa Katoliki nchini humo kupitia baraza la maaskofu lilitoa ujumbe wa tahadhari kwa waumini wake na kukusitiza ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari kwani wao kama kanisa wameona iko haja ya kufanya hivyo.