Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amemuagiza mbunge wa jimbo la Kahama Mjini, Jumanne Mashimba, kuhakikisha anajenga kiwanda cha kuongeza thamani ya mchele jimboni kwake, hali itakayosaidia kuokoa soko la mpunga na kukuza kipato cha wakulima wa mkoa huo.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 28, 2021, Kahama mkoani Shinyanga, wakati akizungumza na wananchi wa mkoa huo na ndipo ilipobainika changamoto ya wakulima kukosa soko la mchele hali iliyopelekea wengine kushindwa hata kununua viatu na madaftari ya watoto wao.
"Mbunge Kishimba anzisha kiwanda hapa cha kufanya 'packaging' ya mchele, hakuna sababu ya kujenga kiwanda Zimbabwe wakati hapa Kahama wanahitaji viwanda, nikija hapa nataka unioneshe kiwanda nitakachokuja kukifungua ambacho umekijenga hapa kwa sababu wewe ni mfanyabiashara na ni mbunge wa hapa", ameagiza Rais Magufuli.
Mbali na hayo Rais Dkt. Magufuli pia ameipandisha hadhi wilaya ya Kahama na kuipa hadhi ya kuitwa Manispaa.