Klabu ya Simba SC imemtambulisha rasmi Kocha Mkuu wa timu hiyo Raia wa Ufaransa Didier Gomes Da Rosa ambaye anachukua mikoba iliyoachwa wazi na Kocha Sven Vandenbroeck aliyekimbilia Morocco.
Kocha Gomes alikuwa kocha wa AL-Merrikh ya Sudan ambayo amevunja mkataba na kuja kujiunga na Mabingwa wa Tanzania Simba Ikumbukwe Al-Merrikh ipo kundi Moja na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyu amesaini Mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa Simba ambaye anauzoefu katika bara la Afrika ambapo amewahi kuzifundisha Klabu za Rayan Sports ya Rwanda, Coton Sports ya Cameroon .
Akizungumza baada ya kusaini kandarasi ya miaka miwili, Kocha Didier Da Rosa amesema amefurahi kufika Tanzania na anaijua vizuri Simba SC pia alikuwa na shauku kuifundisha Klabu hiyo, amesema falsafa yake ya ufundishaji Soka inalingana sana na falsafa ya Klabu ya Simba ya kucheza mpira wa pasi.
"Najua nimekuja hapa lengo kubwa kufanya vizuri na kufika mbali katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pia kutwaa Taji la Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, naamini tutafanya hivyo katika kipindi hiki kifupi, nimefurahi kuja kufundisha timu yenye ushawishi katika Bara la Afrika", amesema Didier Da Rosa.
"Ligi ya Tanzania naijua naifuatilia na najua yupo Mchezaji Medie Kagere namjua nimemfundisha Rayon Sports, Rwanda", ameeleza Didier Da Rosa.
Didier Da Rosa amesema nidhamu ni sÃlaha muhimu ili kufika malengo ya timu na kufika mbali zaidi katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu kwa kipindi cha Mashindano kilichobaki, "Huwezi kufanya vizuri katika Mashindano yeyote kama huna nidhamu, mimi huwa nawapenda sana Wachezaji wangu na napenda wawe na nidhamu pia".
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez amesema wameona ubora wa Kocha huyo baada ya kupitia CV zaidi ya 70 wakati wa harakati za kutafuta Kocha mpya wa Klabu hiyo.
Barbara amesema walikuwa na ushirikiano na baadhi ya Makocha waliowahi kufanya kazi na Makocha hao waliokuwa wanawatafuta baada ya kuondoka Kocha Sven Vandenbroeck baada ya timu kufuzu Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia Barbara amesisitiza Kocha Msaidizi Suleiman Matola ataendelea kuwa sehemu ya Kikosi cha Simba ili kuendelea kuwapa uzoefu Makocha wa Tanzania katika ufundishaji wa Soka.