Taarifa kutoka katika jimbo la Katsina nchini Nigeria zinasema kuwa watu wenye silaha wameishambulia shule ya wavulana iliyopo eneo la Dankara, GSSS Dankara, na kuwateka nyara wanafunzi kadhaa.
Inaarifiwa kuwa wanafunzi 400 hawajulikani walipo baada ya shambulio hilo.
Polisi katika jimbo hilo wamethibitisha uvamizi huo katika mazungumzo na BBC , lakini wanasema hawana taarifa kuhusu watekaji.
Msemaji wa polisi katika jimbo hilo DSP Gambo Isa, amesema kuwa wanafunzi wengine 200 waliokuwa wametorokea maeneo ya misituni , wakati washambuliaji waliipoivamia shule yao wameweza kupatikana.
Aliongeza kuwa kulikuwa na makabiliano baina ya polisi na wavamizi wenye silaha yaliyoyosababisha " kupigwa risasi kwa polisi mmoja lakini hakuuawa ."
Kulingana na msemaji huyo wa polisi , polisi zaidi wamepelekwa katika eneo la tukio ili kukabiliana na wanamgambo hao wenye silaha , na kuongeza kuwa bado wanawasaka.
Wanafunzi walioweza kurejea kutoka mafichoni walielezea wasi wasi mkubwa uliotanda wakati washambuliaji walipoivamia shule yao.
Walioshuhudia tukio hilo wanasema waliwaona washambuliaji wakiwateka nyara wanafunzi na kuondoka nao.
Mwanaume mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe , aliongeza kuwa : "Mtu mwenye silaha alipita mbele yangu na kufyatua risasi na akaingia ndani ya shule na kuwateka wanafunzi kadhaa. Tangu jioni tulipata taarifa kwamba watafanya shambulio na tukawaambia maafisa wa usalama lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. "
Shambulio kama hilo lilitokea dhidi ya wasichana wa shule ya sekondari ya Chibok miaka sita iliyopita . Shambulio hili linakuja siku mbili baada ya kutekwa nyara kwa kiongozi wa kijiji na watu wengine 20 katika eneo lingine la jimbo la Katsina.