Sunday, December 6, 2020

Trump amshinikiza gavana wa Georgia kupindua matokeo


Rais wa Marekani Donald Trump amemshinikiza Gavana wa Republican wa Jimbo la Georgia kumsaidia kupindua ushindi wa Rais mteule Joe Biden jimboni humo.

Katika mfululizo wa ujumbe aliotuma kupitia mtandao wa Twitter, Trump amemtaka mgombea, Brian Kemp kuitisha kikao maalum cha bunge.

Hatua hiyo inakuja saa kadhaa baada ya Trump kuhudhuria mkutano wa kampeni huko Georgia wakati jimbo hilo linajitayarisha katika marudio ya uchaguzi wa seneti.

Kulingana na gazeti la Washington Post, Trump alimuita Gavana, Kemp Jumamosi asubuhi na kumtaka adai kuchunguzwa kwa saini za kura za ambao hawakupiga.

Kemp ambaye hana mamlaka ya kuitisha uchunguzi wa aina hiyo  alikataa ombi hilo, kwa mujibu wa vyanzo vya gazeti hilo.

Katika kipindi chote, Trump amekuwa akidai kuwa kura zilizopigwa kwa njia ya posta zilisababisha kusambaa kwa wizi wa kura lakini hana ushahidi wa kuthibitisho madai hayo.

Rais Trump bado amekataa kukubali kuwa alishindwa katika uchaguzi mkuu akidai kulikuwa na wizi wa kura ingawa hajawahi kutoa ushahidi wowote kuthibitisha kwamba ushindi wa Biden ulitokana na wizi wa kura.

Trump amefungua kesi mahakamani katika majimbo kadhaa lakini hadi kufikia sasa zote zimeshindwa kufaulu.

Jimbo la Georgia lilikuwa ngome muhimu katika uchaguzi huo ambapo Joe Biden aliibuka na ushindi mdogo – ikiwa ni mara ya kwanza jimbo hilo linampigia kura mgombea urais wa chama cha Democrat tangu mwaka 1992.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...