Taasisi za Serikali zimetakiwa kuona umuhimu wa kuzingatia miondombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufika kwa urahisi katika maeneo hayo pindi wanapotafuta huduma katika Taasisi hizo.
Wito huo umetolewa wilayani Kongwa Mkoani Dodoma na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu ambayo hufanyika Disemba 3,kila mwaka yenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu na kujua mahitaji yao.
Mhe Ndugai amesema watu wenye ulemavu mara nyingi wamekuwa wakiachwa nyuma kwenye miondombinu na kuleta usumbufu pindi wanapofika kwenye taasisi hizo kufuata huduma.
Kuhusu mikopo ya walemavu amesema licha ya kuwa nao wanatambulika katika kupatiwa mikopo lakini wamekuwa na masharti magumu likiwemo la kuwataka wajiunge katika vikundi vya watu watano.
"Neno vikundi linaleta matatizo makubwa na kupelekea wengine kushindwa kupata mikopo kutokana na masharti yaliyowekwa" amesema Spika Ndugai
Ameongeza kuwa "Haiwezekani watu wenye ulemavu kulazimishwa kuwa katika makundi wakati unakuta katika sehemu moja labda kuna walemavu wawili,sasa kikunsi kinataka watu watano,hao wengine wanapatikana wapi,suala hili inabidi ulitazame upya,
"Nakubaliana nanyi kwamba masharti siyo rafiki,ila walengwa wanapochukua mikopo hii wahakikishe wanairudisha ili na wengine waweze kupata fursa hiyo,"amesema.
Spika Ndugai ameahidi kuwapa ushirikiano wabunge wanaowakilisha watu wenye ulemavu ili kufanya maisha yao yawe bora zaidi ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini (SHIVYAWATA) Tungi Mwanjala ameiomba Serikali kutoa bure vifaa vya watu wenye ulemavu kutokana na vifaa hivyo kuuzwa bei ghali na hivyo wengi kushindwa kumudu gharama hizo.
Ametaja changamoto zinazowakabili ni pamoja na kutokiwa na miundombinu rafiki hasa katika majengo ya serikali,upatikanaji wa matibabu ,ukosefu wa ofisi kwa wenye ulemavu,kutokiwepo kwa bajeti ya kutosha kwa watu wenye ulemavu na kuwapatia bima ya afya.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dk. Suleiman Selela akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dk.Binilithi Mahenge, amesema ,maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuifikia jamii hasa ya vijijini kutokana na maadhimisho hayo kufanyika wilayani.
Selela amesema licha ya Serikali kuzifanyia kazi changamoto za wenye ulemavu,lakini bado kuna changamoto ambazo mkoa unazifanyia kazi katika kuzitatua.