Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza Waraka wa mwaka 2002 ambao unawataka kutenga asilimia 15 ya mapato yanayotokana na shughuli za Sekta ya Mifugo na Uvuvi na kuzirejesha kwenye sekta hizo ili kuboresha shughuli zake.
Gekul alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro alipotembelea kukagua shughuli za Sekta ya mifugo na uvuvi zinazotekelezwa Wilayani humo Disemba 23, 2020.
Kwa mujibu wa Gekul, mwaka 2002 Serikali ilitoa waraka ambao unaelekeza kuwa Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa mapato yanayopatikana kutokana na shughuli za sekta ya mifugo na uvuvi itengwe asilimia 15 na zirudishwe kwa sekta hizo ili kuboresha huduma kwa mifugo ikiwemo ukarabati wa majosho, minada na kununua chanjo za mifugo.
"Wakurugenzi rejeeni huo waraka ambao unadumu mpaka mwaka 2025 ili mtekeleze kama ulivyoagiza na tukifanya hivyo itasaidia kuboresha huduma za mifugo yetu na tupate mazao bora yanayotokana na mifugo hiyo," alisema Gekul
Aliendelea kusema kuwa miundombinu mingi ya kuhudumia mifugo imechoka akitolea mfano minada ya kuuzia ng'ombe kuwa mingi haina uzio, mifugo inauzwa katika maeneo ya wazi jambo ambalo linachangia upotevu wa mapato ya Halmashauri.
"Najua katika Halmashauri zetu mara nyingi fedha huwa hazitoshi lakini ni muhimu kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na tukifanya hivyo itakuwa rahisi kutenga hizo pesa ili kuboresha sekta za mifugo na uvuvi, hivyo naagiza baada ya kutoka hapa tukatekeleze hilo," alisisitiza Gekul
Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa muelekeo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha majosho yanaboreshwa, minada inakarabatiwa na chanjo zinapatikana kwa urahisi ili wananchi wasihangaike kupata huduma kwa ajili ya mifugo yao.
Pia, aliwataka maafisa mifugo kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili kuzuia upotevu wa mapato kwani makusanyo yakiwa mazuri na huduma za mifugo zitaboreshwa.