Sunday, October 11, 2020

Sudan Kusini: Takriban watu 18 wauawa kwenye mapambano kati ya koo mbili

 


Watu wapatao 18 wamekufa kufuatia mapigano mapya yaliyozuka kati ya koo mbili nchini Sudan Kusini. Kulingana na afisa katika eneo hilo, mapigano hayo yalitokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika jimbo la Warrap, lililopo kaskazini mwa Sudan. 

Kamishna wa eneo hilo Samuel Awan, amesema watu 34 walijeruhiwa kwenye mapigano hayo wakati ambapo uhasama unaongezeka kwenye maeneo ya vijijini nchini humo.

Mapigano hayo kati ya koo mbili zinazopingana yalisababishwa na kuuawa kwa mtu mmoja mnamo siku ya Alhamisi jioni. 

Watu wasiojulikana waliokuwa na silaha walimuua mtu huyo jambo lililozusha lawama kati ya pande mbili hasimu. 

Maafisa wanahofia kuzuka tena kwa mapigano zaidi iwapo serikali haitaingilia kati kwa haraka.

Mnamo mwezi Agosti zaidi ya watu 100 waliuawa katika mkoa huo wa Warrap pale raia walipopambana na jeshi kuhusu zoezi la upokonyaji silaha baada ya askari wa Sudan Kusini wa kikosi cha Ulinzi wa Watu walipojaribu kuwapokonya silaha raia katika mji wa Tonj Mashariki mwa nchi hiyo kama sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa hivi karibuni.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...