Tuesday, October 6, 2020

Njombe: Wananchi wazua gumzo Makaburini, wataka ufafanuzi kifo cha marehemu aliyekuwa mikononi mwa Polisi

 



Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wakazi wa kata ya Mji Mwema halmashauri ya mji wa Njombe,wameibua gumzo Makaburini wakihitaji taarifa ya kifo cha kijana Kelvin Fute (34) mkazi wa kata hiyo aliyekutwa na kifo cha utata wakati akiwa mikononi mwa jeshi la polisi.

Waombolezaji waliofika katika mazishi eneo la Hagafilo walitaka ufafanuzi wa kifo cha kijana huyo ambaye alikuwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuuza msitu usio kuwa mali yake huku wakitaka polisi kushiliki zoezi la kusindikiza kaburini mwili wa kijana huyo.


Kutokana na hali hiyo msemaji wa familia bwana Gideon Stiven Mwautenzi amefafanua sababu za kifo cha kijana wao Kelvin Fute kuwa ni kutokana na mbinu za jeshi la polisi zilizokuwa zikitumiwa na jeshi la polisi katika mahojiano kwa kuwa walibaini katika mwili wa marehemu kuwa na majeraha.

"Mpaka kufikia hapa tumekaa na mkuu wa wilaya tukiwa na wanafamilia wasiopungua arobaini na kuongea kwa kina baada ya kukubaliana mambo mengi tulikwenda Mochwari kutambua mwili wa marehemu,tulichokiona tulimwambia daktari andika amuawa maana yake alichomwa mgongoni na umeme na alivunjwa mguu"alisema Gideon Stiven Mwautenzi

Mwautenzi aliongeza kuwa "Nilipokuwa kwa mkuu wa wilaya nilisema mdogo wangu sikatai kwenye mambo haya ambayo anahisiwa ninamtambua na ninamjua vilivyo lakini kosa ni kumchukua bila kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa,amekufa bila kutoa taarifa na mmeshinda naye kama masaa 24 hili jambo kama mimi mwanafamilia halikai kabisa akilini mwangu"alisema msemaji wa familia


Kwa upande muwakilishi wa jeshi la polisi Insp.Oraity Shomari,amesema kwa kuwa tayari swala la kifo hicho limefika ngazi ya juu hawezi kuzungumza mambo mengi huku akiomba wananchi waweze kushirikiana katika mazishi hayo.

"Kwa hiyo sisi tumekuja kushiriki katika hili swala la msiba na siwezi kuongeza mambo mengi zaidi,ninaomba tumzike salama na kama kuna mambo mengine ya kisheria yapo yanaendelea"alisema Insp.Oraity Shomari

Kutokana na ufafanuzi huo ndipo waombolezaji wakaweza kushirikiana na jeshi la polisi katika mazishi ya kijana huyo.

Michael Lugome ni mchungaji wa kanisa la Anglican aliyeongoza ibada ya mazishi,ametoa wito kwa vijana na jamii kubadilisha mienendo katika maisha yao huku akiomba jeshi la polisi na viongozi wa serikali kuendelea kuongoza kwa kufuata jamii kwa kufuata sheria hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kulinda amani.

"Yupo ambaye amepewa kazi ya hukumu,ninaomba vyombo vya sheria viweke utaratibu mzuri kuleta amani katika nchi yetu,tuna jambo la uchaguzi mbele yetu tusingependa kusikia kuna watu wanaleta shida na migongano tunaomba sana tusaidiane kutafuta amani,na vijana tunaomba hebu turekebishe hayo mapito yenu"alisema Michael Lugome

Marehemu Kelvin Fute mjasiriamali wa mtaa wa Lunyanywi alifariki mnamo tarehe 2 0ctobar 2020 akiwa mikononi mwa jeshi la polisi huku akiwa ameacha mke na watoto wawili.Hata hivyo jeshi la polisi limeshirikiana na waombolezaji katika mazishi ya kijana huyo pamoja na ghalama zinazohusu msiba huo.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...