Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba (kulia), kushoto ni mfano wa kisu cha moto
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Meckrida Masesa (25), mkazi wa Chela wilayani Kahama kwa kosa la kumjeruhi mdogo wake mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa), mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Baloha kwa kumuunguza sehemu za usoni, mashavuni na mapajani kwa kutumia kisu cha moto akimtuhumu kuchepuka na shemeji yake.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokea Septemba 28,2020 majira ya saa kumi na moja jioni katika kijiji na kata ya Chela, halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama.
Amesema mhanga alijeruhiwa kwa kuunguzwa na kisu cha moto na mtuhumiwa huyo ambaye ni dada yake wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa.
"Chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi baada ya dada yake huyo kumtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na shemeji yake ambaye ni mume wa mtuhumiwa huyo aitwaye Joseph Masolwa ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Chela",ameeleza Kamanda Magiligimba.
"Mtuhumiwa alikiweka kisu hicho kwenye moto kwanza na kisha kuanza kumjeruhi mhanga. majeruhi anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Lunguya na hali inaendelea vizuri",amesema.
Kamanda Magiligimba anatoa wito wenzi/wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala wapeleke matatizo/migogoro yao ya ndoa kwenye ofisi za dawati la jinsia na watoto, viongozi wa dini,ofisi za ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao.