MGOMBEA ubunge Iramba Mashariki Mkoa wa Singida kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Mwigulu Nchemba, ameanza kumchokonoa Tundu Lissu, mgombea urais kupitia Chadema na Lazaro Nyalandu, mgombea ubunge wa Singida Kaskazini.
Akizungumza kwenye kampeni za Dk. John Magufuli, mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho katika Uwanja wa Bombadier mkoani Singida leo tarehe 1 Septemba 2020 amesema, wawili hao hawana uzalendo.
Bila kuwataja majina, Mwigulu alimnanga Nyalandu kwamba, alipokuwa waziri (Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne) alikuwa akienda Ulaya kunyoosha suti zake huku Lissu akisema amerejea nchini baada ya kupewa 'advance' (malipo ya awali).
Lissu ndiye aliyerejea nchini akitokea kwenye matibabu nchini Ubelgiji, ni baada ya watu wasiojulikana kushamabuliwa kwa risasi 'Area D,' jijini Dodoma tarehe 7 Septemba 2017.
Mara kadhaa Lissu alinukuliwa na vyombo vya habari akiwa ughaibuni, kwamba alishindwa kurudi Tanzania kwa kuwa sio sehemu salama kwake.
"Wengine wanakuja hapa wanajifanya watoto wa Singida, hawana uzalendo hata na wana Singida. Kuna mmoja tulikuwa mawaziri wote, hata suti zake alikuwa anaenda kunyoosha Ulaya, hana uchungu na Singida.
"Mwingine alisema Tanzania sio salama, sasa hivi amekuja sababu 'advance' amechukua baada ya uchaguzi tu atasema, Tanzania haiko salama, ataondoka," amesema Dk. Mwigulu.
Dk. Mwigulu ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, amewataka Watanzania kumchagua Rais Magufuli. "Ioneeni huruma Tanzania, wale wagombea wengine wote mimi nawafahamu na nikiangalia janja janja yao, naona hata 'advance' wamechukua, nchi yetu itauzwa mkimuacha Dk. Magufuli," amesema Dk. Mwigulu.