MTOTO mwingine wa kike mwenye umri wa siku tatu, ameopolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye choo cha Zahanati ya Mshikamano wilayani Ngara mkoani Kagera akiwa hai.
Hilo ni tukio la pili kutokea wilayani humo, kwani Mei 21 mwaka huu, mtoto Isabela aliopolewa akiwa hai kwenye choo cha Shule ya Msingi Murganza wilayani humo na jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Hamis Dawa, amesema walipata taarifa ya kutupwa kwa kichanga hicho katika choo cha Zahanati ya Mshikamano kupitia kwa Jeshi la Polisi wilayani humo.
"Baada ya taarifa hiyo, tuliwatuma askari wawili ambao ni ZM 3338 Sajenti Bahati Rudisha na FC 3802 Amos Mwita, ambao walifanikiwa kumuokoa mtoto huyo akiwa hai.
"Mtoto huyo tumemkabidhi kwenye Hospitali ya Mshikamano kwa ajili ya matibabu wakati huo Jeshi la Polisi likiendelea kumtafuta mama wa mtoto huyo aliyemtupa kwenye shimo la choo," alisema kamanda Hamisi Dawa.
Kwa mujibu wa Kamanda Dawa, kichanga hicho ambacho kilikuwa bado hakijakatika kitovu, kiliopolewa katika choo hicho kilichokuwa kinatumika, hivyo baada ya askari hao kubomoa mfuniko wa choo, walikiona kikiwa kinaelea.
"Mtoto hakukutwa na majeraha, bali alikuwa na afya njema, hivyo wahudumu wa afya hospitalini, wanaendelea kumfanyia uchunguzi wa kitabibu
"Tunashirikiana na watu wa Ustawi wa Jamii na wahudumu wa afya kitengo cha afya ya uzazi, ili kuweza kutoa elimu kwa akina mama ambao ndiyo wanaobeba ujauzito, jinsi ya kulea na kukabiliana na changamoto za kifamilia zinazowasababishia kutenda ukatili kwa watoto kama huu," alisema Kamanda Dawa.
Source