Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya,akizungumza wakati wa kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya,akisisitiza jambo kwenye kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani,akitoa neno kwenye kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt.Benson Ndiege,akitoa taarifa wakati wa kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya.
Afisa Ushirika Mkuu Bi.Veneranda Mugoba,akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya mara baada ya kumaliza kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakifatiliwa Hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati wa kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma
.............................................................................................
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kuendelea kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Ushirika nchini katika Nyanja za Kilimo, ufugaji, uvuvi, madini kwani sekta hizo zimeendelea kuchangia uchumi wa Taifa.
Umuhimu wa Sekta hizo umetokana na kuwaunganisha wanachama katika uzalishaji, ukusanyaji mazao na upatikanaji wa masoko.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao cha Makamishna na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika Jijini Dodoma.
Kusaya amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imefanya na inaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha Ushirika nchini.
Serikali imejikita katika kuimarisha Usimamizi na Utawala Bora katika Vyama vya Ushirika, kupitia Sheria ya Ushirika Na 6 ya Mwaka 2013 na Kanuni za mwaka 2015.
Aidha Kusaya amesema kuwa usimamizi wa vyama unaanzia kwa mwanachama mwenyewe, juhudi zimeelekewa kwenye Mafunzo kwa viongozi wa vyama vya ushirika na wanachama wao kupitia mpango kazi uliotolewa naTume ya Maendeleo ya Ushirika.
Pia serikali imeendelea kuchukua hatua kupitia vyombo vya usalama pale ambapo kuna wizi na ubadhilifu kwenye vyama.
Nia ya serikali ni kurudisha Imani ya wananchi juu ya ushirika.
"Kwa hatua hizi kumekuwepo na mabadiliko chanya kwenye ushirika ambapo wananchi wameendelea kuanzisha na kujiunga katika vyama vya Ushirika wa aina mbalimbali ikiwemo vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) hatua ambayo itawezesha kupanua shughuli zao za uzalishaji mali na kuongeza kipato na hatimaye kupunguza umasikini.
Pia, kwa sasa wakulima wanauza mazao yao kupitia mfumo wa Ushirika. Mfumo ambao umesaidia kuimarisha ubora wa mazao, kupatikana kwa bei za ushindani, uhakika wa vipimo vya mazao," alisistiza Bw.Kusaya
Mfumo wa Ushirika umesaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji na uhakika wa mapato ya Halmashauri za Wilaya husika.
Kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa(TMX) na bodi za mazao, masoko ya mazao ya kimkakati na mazao mchanganyiko yameendelea kuimarika kama vile mazao ya tumbaku, choroko, kahawa, pamba, ufuta, kokoa na mbaazi yaliuzwa kupitia mfumo wa ushirika katika msimu wa 2019/20 kwa thamani ya Shilingi trilioni 2.7.
Awali akiwasilisha Mafanikio na changamoto za Tume, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ameeleza kuwa Vyama vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vimeongeza mikopo kwa wanachama wake kutoka Shillingi Billioni 854 mwaka 2017 hadi kufikia Shillingi Trillioni 1.5 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia.
Ushirika ni Sekta ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa vijana na wananchi kwakuwa ni sekta ambayo inagusa maisha na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Tume imeendelea kusimamia masuala ya ajira na kuwezesha wananchi Zaidi ya 90,090 kupata ajira katika vyama vya Ushirika zikiwemo ajira za kudumu, mkataba na za msimu hadi kufikia Juni 2020 ikilinganishwa na ajira 32,668 mwaka 2018," alisema Dkt. Ndiege
Kwa upande wake Kamishna Salome Tondi, amesema Sekta ya Ushirika inaweza kuendelea kukua na kuimarika kwa kuhakikisha elimu ya Ushirika inawafikia wengi katika jamii.
Tondi alifafanua kuwa elimu ni moja ya nyenzo muhimu inayoweza kuwakomboa wanaushirika akitoa mfano wa masuala ya haki na wajibu wa wanaushirika, taratibu za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika, taratibu za uchaguzi wa viongozi wa Vyama vya Ushirika na masuala mengine mengi.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilikuwa ni fursa ya Makamishna kukaa kwa pamoja na watumishi wa Tume kufanya tathmini ya masuala mbalimbali ya Ushirika katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2017 baada ya uteuzi wao kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.