Na Angela Kibwana, Morogoro Na P. Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro nchini Tanzania amefunga Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mtakatifu baada ya kuwasiliana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania.
Kuanzia tarehe 27 Aprili 2020 Kanisa la Parokia ya Modeko limefungwa na halitaweza kutumika kwa sasa hadi pale, Tabernakulo mpya itakapowekwa wakfu.
Ibada hii inatarajiwa kuadhimishwa wakati wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai.
Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo.
Padre Nikodemas Masong, Paroko wa Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki la Morogoro amesema, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi tarehe 27 Aprili 2020 walivamia na kuvunja mlango wa Kanisa la Parokia ya Modeko na kufanikiwa kuiba Tabernakulo iliyokuwa inahifadhi Ekaristi Takatifu na kutokomea mahali kusikojulikana.
Walivunja pia milango ya ofisi za Parokia na kufanikiwa kuiba kiasi cha shilingi laki tatu na nusu, mali ya Chama cha Watumishi wa Altare Parokiani hapo. Walifanikiwa pia kuiba "Mixer" inayotumika kwa ajili ya mawasiliano Parokiani hapo.
Familia ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Morogoro imesikitishwa sana na kufuru hizi dhidi ya mahali na mambo matakatifu yanayogusa undani wa imani ya watu.
Via Vatican News