Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwandu Chalya (75) na mke wake Gigwa Kwangu (70) wakazi wa kijiji cha Mwamasololo, kata ya Sekebugoro wilayani Kishapu wamenusurika kufa baada kukatwa na kitu chenye ncha kali 'panga' na mkwe wao 'Mkwilima' Masele Boniface akilipiza kisasi kwa sababu wamekataa asirudiane na mke wake aliyetengana naye kwa kupeana talaka mahakamani.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea leo Aprili 29,2020 majira ya saa nane usiku katika kitongoji cha N'halange, kijiji cha Mwamasololo, kata ya Sekebugoro, tarafa ya mondo, wilaya ya Kishapu.
Amesema Mwandu Chalya (75) pamoja na mke wake aitwaye Gigwa Kwangu (70) wote wakazi wa Mwamasololo walijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na mkwe wao 'Mkwilima' Masele Boniphace wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao.
"Chanzo cha tukio hili ni chuki /kulipiza kisasi baada ya wazazi wa mke wake aitwaye Emiliana Mwandu (31) mkazi wa Mwamasololo kumkataza kurudiana na Masele Boniface baada ya kutengana kwa kupeana talaka mahakamani mnamo tarehe 06/05/2019 kwa sababu za ukatili aliokuwa akifanyiwa na mtuhumiwa kwa kupigwa hadi kupoteza fahamu kipindi hicho 2019",ameeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda Magiligimba amesema mtuhumiwa alikimbia mara baada ya tukio hilo na juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuacha kabisa tabia ya kujichukulia sheria mkononi na inapotokea kutoridhika na maamuzi ya mahakama ni vyema kuchukua hatua ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya mahakama badala ya kujichukulia sheria mkononi.