Monday, February 10, 2020

MAKATIBU WASTAAFU WA CCM KINANA NA MAKAMBA WATINGA OFISI ZA CCM KUHOJIWA


Makatibu Wakuu Wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Yusuf Makamba na Ndg. Abdulrahaman Kinana leo Februari 10, 2020 wamefika katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam kuitikia wito wa Kamati ndogo ya Usalama na Maadili inayoongozwa na Ndg. Philip Mangula. Pichani Ndg. Yusuf Makamba akiagwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Bashiru Ally Kakurwa baada ya kuitikia wito wa Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili ya CCM.
Pichani Ndg. Abdulrahaman Kinana akiwa ofisini kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Ndg. Philip Mangula baada ya kuitikia wito wa kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili ya CCM.

Makatibu wakuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba leo Jumatatu Februari 10, 2020 mchana walifika katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam na kupokelewa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula pamoja na katibu mkuu, Dk Bashiru Ally.

Kufika kwao huenda kukamaliza mjadala wa kinachoendelea juu yao baada ya taarifa ambazo hakuna upande uliozithibitisha iwapo wamejiuzulu uanachama wa CCM na kupoteza sifa za kuhojiwa.

Taarifa za Kinana na Makamba kujiuzulu zilisambaa mitandaoni na ilielezwa kuwa barua zao za uamuzi huo wameziwasilisha ofisi ya katibu mkuu wa CCM zikiambatanishwa na kadi zao za uanachama.

Baada ya kuwasili baadaye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akielezea kufika kwao.

"Wamefika kuitikia wito wa kamati ndogo ya usalama na maadili inayoongozwa na ndugu Mangula. Kinana na Makamba wamefika katika ofisi hizo mchana na kupokelewa na Mangula na Dk Bashiru," amesema Polepole katika taarifa hiyo.

Kinana, Makamba na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe waliitwa mbele ya kamati ya maadili baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayewachafua.

Membe alifika mbele ya kamati hiyo yenye wajumbe wanne Alhamisi iliyopita Februari 5, 2020 makao makuu ya CCM Dodoma, alihojiwa kwa zaidi ya saa 5 na baadaye akawaeleza waandishi wa habari jinsi alivyofurahishwa na mahojiano hayo na kuwa Mungu alimpa ujasiri wa kuzungumza kile alichotaka kuiambia kamati hiyo na hakuyumba wala kuyumbishwa.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...